0
Kwa mujibu wa gazeti la Champion, Azam FC
inataka kuachana na fowadi wao, Kipre Tchetche,
kutokana na utovu wa nidhamu aliouonyesha kwa
kutojumuika kambini mpaka sasa, ikiwa ni wiki
moja.
Taarifa za chinichini zinadai chanzo cha yote,
fowadi huyo raia wa Ivory Coast analazimisha
kutaka kuondoka kikosini hapo na kwamba
amekuwa akirubuniwa na timu za ukanda huu wa
Afrika Mashariki.
Yanga ndiyo imehusishwa zaidi na kumshawishi
mchezaji huyo bora msimu 2013/14, wakitaka
achukue nafasi ya Donald Ngoma ambaye amezidi
kuitoa udenda Mamelodi Sundown ya Afrika
Kusini.
Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba amekiri
Kipre kutofika kambini mpaka sasa na kwamba
katika mawasiliano yao hajatoa sababu za msingi
za kuchelewa, hali inayowapa wasiwasi
analazimisha kuondoka.
Kawemba ameweka bayana kuwa iwapo kweli kuna
timu inamrubuni, basi ijitokeze kumnunua lakini
akasisitiza thamani yake ni dola 150,000 (Sh
milioni 322.1).
"Hajafika mpaka sasa na kila tukiwasiliana naye
anatuambia anakuja leo, kesho na hafiki. Sasa
hatujui anawaza nini lakini ifahamike bado ana
mkataba na Azam wa mwaka mmoja na kila kitu
juu ya mikataba yake tunacho sisi.
"Kama kweli anataka kuondoka, thamani yake ipo
wazi. Dola 150,000 na bahati nzuri wachezaji wetu
wote kila mmoja thamani yake ipo kwenye
mkataba anaousaini.
"Iwapo kuna timu inamtaka, ije inajua kabisa
thamani yake ni ileile iliyo kwenye mkataba wake,"
alisema Kawemba na kusema kuwa Yanga
hawajajitokeza hadharani.
Licha ya hivyo, Kawemba akasisitiza kuondoka
ama kutoondoka kwake hilo wanaliacha mikononi
mwa Kocha Zeben Hernandez.

Chapisha Maoni

 
Top