0
Klabu za Simba na Yanga bado zinalia na mkataba
kiduchu wa udhamini wa Azam Media walioingia
na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), juzi.
Azam na TFF zimeingia mkataba wa Sh bilioni 23
kwa mwaka wa haki za matangazo ili kurusha
‘live’ mechi za Ligi Kuu Tanzania bara itakayoanza
rasmi mapema mwezi ujao.
Mwenyekiti wa Simba, Evans Aveva akizungumzia
mkataba huo jana alisema, “Kwa klabu ya Simba
Sh milioni 126 kwa mwaka ni ndogo mno,”
alisema.
Hata hivyo, Aveva alisema kuwa licha ya fedha
hizo kuwa ndogo ni nafuu kiasi kwa vile hakuna
kampuni ambayo ilikuwa tayari kudhamini ligi hiyo
kwa kuzipa klabu Sh milioni 200 kwa mwaka.
“Tenda ilikuwa ya wazi si kama ambavyo
inaaminishwa kwenye mitandao ya kijamii, mara ya
kwanza ilitangazwa na Kampuni ya TING ilishtaki
TFF kwenye ‘fare competition’ mchakato ukafutwa
na kuanza upya. Kampuni zinakuja zinataka
kudhamini kwa Sh bilioni 7 nyingine Sh bilioni 10
lakini hakuna hata moja iliyofikia Sh bilioni 23…
“Si mchakato wa pili hakukuwa na kampuni
iliyokuwa tayari, Azam wamejitahidi, japokuwa
ukiangalia uendeshaji wa timu zetu na gharama
tunazotumia kiwango cha fedha wanachotoa ni
kidogo ila ni nafuu tofauti na hao wengine ambao
wanataka kutoa kidogo zaidi halafu wanabaki
wanalalamika,” alisema Aveva.
Mmoja wa viongozi wa klabu hiyo ya Msimbazi
akiuchambua mkataba wa Azam alisema, “Klabu
zinanyonywa, tangu Azam inaonesha mpira
mapato uwanjani yamepungua inafika kipindi
Simba mapato ya mlangoni inapata Sh milioni 5
ukiondoa mechi dhidi ya Yanga na Azam ambazo
zinaingia Sh milioni 60.
“Udhamini wa Azam wa Ligi Kuu Sh milioni 360
udhamini wa Azam, Simba Tv Sh milioni 100 jumla
ni Sh milioni 460, ukijumlisha na Sh milioni 300
za udhamini wa TBL, Simba inakusanya Sh milioni
760 kwa mwaka, gharama za uendeshaji Simba
pamoja na mishahara ya wachezaji inafika Sh
bilioni 1.6 kwa mwaka, ukiangalia hii mikataba
kwa jicho la tatu klabu zinanyonywa,” alisema.
Kwa upande wa Yanga ambao walisusa udhamini
wa Azam tangu mwaka 2013 ulipoanza na hivyo
kuziacha zaidi ya Sh milioni 300, kupitia kwa
Katibu Mkuu wake Baraka Deusdetit alisema kuwa
msimamo wa klabu yao upo pale pale na
wataendelea kusimamia hoja zao kuwa
haiwezekani wakapata udhamini wa Sh milioni 126
kwa mwaka sawa na klabu nyingine za Ligi Kuu,
wakati mechi zao wamekuwa wakiingiza zaidi ya
fedha hizo.
Katika madai ya Yanga walishaweka wazi kuwa
haijawahi kutokea katika ligi ya mpira wa miguu ya
kisasa kulazimishwa kwa Klabu inayoshindana
katika ligi kuachia haki zake za urushwaji wa
michezo zichukuliwe na chombo cha habari cha
Klabu ya upinzani.
Yanga walitaka pia mgawo huo uzingatie klabu
zenye mashabiki wengi ndio wapate mgawo
mkubwa tofauti na klabu nyingine.
Hata katika mgawanyo ambao Yanga walikuwa
wanaupigania wa timu inayoongoza ligi na ile
inayoshika mkia katika mkataba mpya wa sasa wa
Azam wamezingatia hilo kwa kuboresha kipengele
hicho ambacho mgawanyo wa awamu ya mwisho
utazingatia timu inayoongoza kwenye msimamo
wa ligi ambayo itaongezewa Sh milioni 40 zaidi.
Kwa upande wa African Lyon, kupitia kwa
mkurugenzi wake Rahim Kangezi alisema
“Mkataba ni mzuri, unajua unapopiga kelele fedha
ndogo angalia miundo mbinu ya viwanja vyetu
kwanza, Azam wanajitahidi sana viwanja vyetu ni
vibovu, Kampuni kama Super Sports haiwezi
kudhamini ligi kwa Sh bilioni 23 kwa viwanja
vibovu kama vyetu,” alisema.
Mmoja wa viongozi wa klabu moja ya Ligi nchini,
aliponda msimamo wa Yanga kwa madai kuwa
viongozi wake si wa kibiashara kwa vile
wanapishana na fursa ambazo siku za mbeleni
watakuja kuzijutia.
“Kambi ya kujiandaa na mechi ya Mo Bejaia na TP
Mazembe Uturuki, iligharimu Sh milioni 500, sasa
hivi wameweka kambi Kunduchi kwa ajili ya
Medeama gharama zinafikia karibu Sh milioni 300,
mchezo wa TP Mazembe walikuwa waingize Sh
milioni 600 lakini matokeo yake hawakuambulia
kitu kwa klabu ambayo inajali maendeleo yake,
fedha zote hizo walikua na uwezo wa kukarabati
hata uwanja wao wa mazoezi,” alisema.
“Anayekwamisha Yanga ni mtu mmoja tu na
mpaka wakija kuamka muda utakuwa umewatupa
mkono,” alisema kiongozi huyo.
Kwa upande wake Mkuu wa kikosi cha JKT Ruvu,
Meja Charles Mbuge alisema udhamini wa Azam
Media hautakiwi kubezwa, kwa kuwa ndio pekee
waliojitokeza kukuza soka la Tanzania.
Meja Mbuge alisema anaipongeza kampuni hiyo
kwa kutoa udhamini ambao haubagui timu yoyote
tofauti na kampuni nyingine ambazo zimelenga
kudhamini baadhi ya timu ilimradi kujitangaza na
sio kusaidia kukuza soka.
“Udhamini wa Azam umeonesha nia ya kusaidia
kukuza soka letu, na sisi tunapongeza kwa sababu
Tanzania leo tuna makampuni mangapi na
yameshindwa kusaidia, mengi yana nia ya
kujitangaza tu,”alisema.
Alisema kampuni hiyo inapaswa kuungwa mkono
kwa kujaribu kuleta mapinduzi ya soka nchini.

Chapisha Maoni

 
Top