Baraza la vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), limeapa kwenda mkoani Dodoma kusaidia jeshi la polisi kuzuia mkutano
mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa mujibu wa taarifa iliyoripotiwa na mtandao wa Mwanahalisi Online.
Kiongozi mmoja mwandamizi wa BAVICHA makao makuu ameuambia mtandao huo kuwa uamuzi wa
wao kwenda Dodoma uko palepale.
“Tumeshaamua kwenda Dodoma na hakuna yeyote anayeweza wa kutuzuia. Uamuzi wetu uko palepale
na tutatekeleza kila ambacho tumepanga,” ameeleza.
Mkutano mkuu wa CCM umepangwa kufanyika mkoani Dodoma wiki mbili zijazo. Unatarajiwa
kumchagua John Pombe Magufuli, kuwa
mwenyekiti wa taifa wa chama hicho.
Msimamo mkali wa kiongozi huyo wa BAVICHA umefuatia uamuzi wa mwenyekiti wa taifa wa
chama hicho, Freeman Mbowe, kuzuia vijana wa
Chadema kwenda Dodoma kukabiliana na CCM.
Mbowe alitoa kauli hiyo jana Jumapili, kufuatia
kuwapo kwa taarifa kuwa jeshi la polisi nchini, limeapa kupambana na viongozi na wafuasi wa
Chadema, ikiwa watafika mkoani humo kuzuia mkutano wa CCM.
Chadema kimeamua kuchukua hatua ya
kukabiliana na CCM baada ya jeshi la polisi kuzuia mikutano ya ndani ya chama hicho; mikutano ya
hadhara na mahafali yaliyopangwa kufanywa na
Umoja wa Wanavyuo wa Chadema (CHASO), katika baadhi ya mikoa.
Kauli ya Mbowe imepingwa na baadhi ya vijana katika maeneo mbalimbali, ikiwamo mkoani Arusha, ambako uongozi wa mkoa umekabidhi
kwa BAVICHA kiasi cha Sh. 5 milioni kwa ajili ya kwenda Dodoma.
Miongoni mwa mahafali ya Chadema
yaliyovurumishwa na polisi, ni pamoja na yale yaliyofanyika mkoani Dodoma ambako mgeni rasmi alikuwa waziri mkuu mstaafu, Frederick
Sumaye.
Mahafali ya Dodoma yalitarajiwa kufanyika katika
hoteli ya African Dreems, yaliporomoshwa na polisi
kwa kutumia mabomu ya machozi, silaha za moto
na gari moja la maji ya kuwasha.
“Upole wa Mbowe na Edward Lowassa, ndiyo uliosababisha tukaibiwa kura na kushindwa kuandamana. Katika hili, hatuko tayari kumsikiliza
yeyote,” ameeleza kiongozi huyo.
Anasema, “…kama Mbowe ameshindwa kuongoza chama basi ni vema akaamua kukaa pembeni na
kuwacha wenye uwezo na ujasiri wa kutenda.
“Kama anaogopa kuwekwa ndani basi aache kabisa siasa hadi watakapopatikana polisi wapole atarudi
kuwa mwenyekiti.”
Akiongea kwa uchungu kiongozi huyo mwandamizw wa Chadema anasema, “tunataka kwenda Dodoma
ili azima yetu itimie. Ni lazima polisi na CCM wafahamu kuwa nchi hii siyo mali ya genge la watu wachache. Nasi ni umma ambao unapaswa
kutendewa haki.”
Katika mitandao ya kijamii kumesheheni mijadala inayopinga kauli na msimamo wa Mbowe wa
kuwazuia BAVICHA kwenda Dodoma na wengine kufikia hatua ya kumshambulia.
Baadhi ya waliojitokeza kupinga uamuzi huo wa
Mbowe, ni viongozi wenzake wa Kamati Kuu (CC), Baraza Kuu la taifa (BKT), wabunge, madiwani na
viongozi wa mikoa.
Hatua ya polisi kuzuia mikutano ya hadhara ilifuatia kauli ya Magufuli, aliyotangaza zuio la jumla la kufanyika mikutano ya kisiasa ya hadhara
na ya ndani na kusema, “wanaotaka kufanya siasa
wasubiri hadi mwaka 2020.”
Mwanahalisi Online
Chapisha Maoni