0

Eneo la uwanja ambalo Mwenyekiti wa Yanga,
Yusuf Manji ameipa klabu hiyo linadaiwa kuwa na
mgogoro.
Manji juzi alitoa eneo la hekari 715 lililo ufukweni
mwa Bahari ya Hindi, Gezeulole, Kigamboni kwa
ajili ya kujenga uwanja.
Habari zilizopatikana Dar es Salaam jana zilisema
eneo hilo lipo kwenye mgogoro wa ardhi na
Kampuni ya mafuta ya Lake Oil. Eneo hilo si lote
mali ya Manji bali kuna sehemu nyingine
inamilikiwa na Lake Oil.
Akihojiwa na gazeti la HabariLeo jana, mmoja wa
wakurugenzi wa Lake Oil, Khalid Hassan maarufu
‘Peter Dau’ alisema ameshangazwa kuona Yanga
wamekabidhiwa eneo lote hilo wakati kuna sehemu
yao pia.
“Inawezakana Manji amepitiwa kwa kusahau kuwa
eneo hilo sio lote lake, kuna sehemu yetu,
tumeona leo (jana) kwenye vyombo vya habari
imetushangaza,” alisema Hassan.
“Sisi tunawasiliana na wanasheria wetu, vielelezo
vyote tunavyo kuwa eneo hilo sisi tumeuziwa,
tunachofanya tutatuma wakaguzi wakaangalie
mipaka yetu kabla hatua nyingine zaidi za kisheria
kuchukuliwa,” alisema.
“Sisi ni wafanyabiashara, naamini kabisa Manji
anaelewa sehemu ya uwanja huo sio wake, sidhani
kama tutashindwa, natumaini tutalimaliza kwa njia
ya amani,” alisema.
Juzi, Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo chini ya
Fatma Karume walikabidhiwa eneo litakalojengwa
uwanja wa Yanga lililopo Gezaulole, Kigamboni.
Eneo hilo ambalo Manji inadaiwa aliuziwa na
Shirika la Taifa la Kilimo na Chakula (NAFCO), kwa
upande wa Lake Oil walidai kuwa hawajauziwa na
Nafco wameuziwa na mtu mwingine ambaye hata
hivyo hawakutaka kumtaja na pia kuweka wazi
ukubwa wa eneo ambalo wanadai wanalimiliki.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa Manji baada ya kuuziwa
eneo hilo, aliliacha kwa muda mrefu bila
kuliendeleza, ndipo watu wengine wakavamia na
hata kuuza baadhi ya maeneo.
Jitihada za kumpata Manji hazikuzaa matunda
baada ya simu yake ya mkononi kuita bila majibu
na hata Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit
hakupatikana kulizungumzia hilo baada ya
kutopokea simu pia.
Gazeti la HabariLeo lilizungumza na mjumbe wa
Baraza la Wadhamini la Yanga Dk Jabir Katundu
ambaye ni miongoni mwa waliohudhuria hafla ya
makabidhiano juzi ambaye alisema hawajui lolote
kuhusu hilo.
“Sisi tumekabidhiwa eneo hatujui kama lina
mgogoro lakini Manji kesharudi kutoka safari hivyo
tutalipeleka suala hili kujua undani wake na
kuangalia namna atakavyolishughulikia,” alisema.



Like Page ya Facebook Africa Newss Sports Posted: ⚽ Africa News Sports2

Chapisha Maoni

 
Top