Timu ya Lipuli FC imesaini mkataba wa udhamini wa miaka miwili wenye
thamani ya Sh.35 milioni na kampuni ya Speshoz.
Katika mkataba huo, timu hiyo itapatiwa vifaa mbalimbali vya michezo sambamba na kusimamiwa mauzo ya bidhaa zenye nembo yake.
Mkurugenzi wa Speshoz, Jeffrey Jessey alisema kuwa nia yao ni kusaidia maendeleo ya
mpira wa miguu Tanzania.
"Kimsingi tunatambua kuwa mchezaji anapocheza huku akiwa na vifaa vyenye ubora, anakuwa huru uwanjani na ataonyesha kiwango chake na kuisaidia timu ifanye vizuri.
Kupitia mkataba huu, tutawapatia jezi za mechi na mazoezi, sare pamoja na viatu vya kuichezea
ambavyo tunaahidi vitakuwa na ubora wa hali ya juu huku pia tukisaidia kusimamia mauzo ya bidhaa hizo kwa mashabiki, " alisema Jessey.
Mwenyekiti wa Lipuli, Abuu Majeki aliwataka mashabiki na wanachama wa timu hiyo kudumisha umoja na mshikamano ili kuvutia wadhamini wengine zaidi.
"Udhamini huu tulioupata sio mdogo na una maana kubwa kwetu kama inavyofahamika kuwa vifaa vya michezo vina gharama kubwa hivyo ujio wa kampuni kama hii katika kutudhamini lazima sisi kama Lipuli tuwashukuru sana.
Tunachowaahidi ni kuwa tutaulinda mkataba huu na kuhakikisha tunatengeneza mazingira bora kwa wadhamini wetu ili kufungua milango kwa wadhamini wengine zaidi waje kutuunga mkono, " alisema Majeki.
Lipuli inakuwa timu ya pili kupata udhamini kati ya tatu zilizopanda Ligi Kuu msimu ujao baada ya Singida United kupata udhamini wa mwaka mmoja na kampuni ya SportPesa.
Chapisha Maoni