Maxime, ameiambia Yanga, ili akubali kuhamia kwao wampe nafasi ya ukocha mkuu ambayo kwa sasa inashikiliwa na Mzambia George Lwandamina
Kocha wa Kagera Sugar Mecky Maxime, ameiambia Yanga , ili akubali kuhamia kwao wampe nafasi ya ukocha mkuu ambayo kwa sasa inashikiliwa na Mzambia George Lwandamina.
Maxime amesema kwa uzoefu aliokuwa nao hataki kufanya kazi kwa cheo cha kocha msaidizi na miaka mitano aliyofanya kazi kama kocha mkuu matunda yake yameonekana hivyo kama Yanga wanamuhitaji kwa ajili ya kuwa msaidizi ni bora akabaki kuendelea kuifundisha timu yake ya Kagera.
"Tupo kwenye mazungumzo na Yanga, lakini msimamo wangu ni kuwa kocha mkuu, na siyo msaidizi najiamini nina uwezo na ndiyo maana nafundisha timu kubwa kama Kagera na kumaliza nafasi ya tatu,"amesema Maxime.
Kocha huyo ambaye ni mshindi wa tuzo ya kocha bora wa msimu uliopita amesema, klabu nyingi za Tanzania zimekuwa haziwaheshimu makocha waza kiasi cha kuwafanya waonekana kama hawana taaluma kumbe ni tofauti na uhalisia uliopo.
Maxime amesema kwa elimu aliyokuwa nayo anaamini anauwezo wa kuifundisha Yanga na kufanya vizuri kwenye michuano yote watakayoshiriki na hiyo kwake itakuwa ni hatua kubwa kumfanya ajulikane nje ya mipaka ya Tanzania.
Mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars, amesema ataendelea kusimama kwenye misingi yake ya kuwa kocha mkuu na kama Yanga wanaona hilo haliwezekani atabaki Kagera kuendelea kuinoa timu hiyo.
Yanga wanamuhitaji Maxime, kuwa msaidizi wa George Lwandamina, na wanampango wa kuachana na kocha msaidizi aliyepo sasa Juma Mwambusi.
Chapisha Maoni