Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia ametetea uamuzi wake ongezeko idadi ya wachezaji 10 wakigeni kwa klabu za Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Awali wachezaji wa kigeni walikuwa 7, lakini Shirikisho hilo lenye dhamana ya soka nchini liliongeza mpaka kufikia idadi ya wachezaji 10 kuanzia msimu ujao.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Mikutano katika ofisiza Shirikisho hilo, Karia alifafanua namna ambavyo kanuni hiyo ilivyopitishwa mpaka kufikia makubaliano.
“Huko nyuma kulikuwa na migogoro mingi juu ya kutoshirikishwa kikamilifu kwa timu wakati wa upitishaji kanuni, Ili kuondoa migogoro hiyo TFF iliamua kuwa mchakato wa kanuni mbali na kushirikisha wadau wengine lakini klabu zipewe uzito katika masuala yanayohusu kanuni za ligi zetu,” alisema Karia.
Karia alifunguka zaidi kwa kusema klabu za ligi kuu kupitia aliyekuwa mwenyekiti wao wa bodi ya ligi waliitisha kikao Juni 30,2018 katika ukumbi wa mikutano uwanja wa Taifa kuzungumzia masuala kadhaa likiwemo suala la kanuni mpya za Ligi Kuu.
“Baada ya kikao cha Bodi ya Ligi walileta mapendekezo ya kanuni mbalimbali kwa kamati ya Utendaji ya TFF ili yapitishwe, moja ya mapendekezo yao ilikuwa ni mabadiliko ya kanuni ya 57, ambapo walipendekeza ongezeko la wachezaji wa kigeni kutoka saba mpaka wachezaji 10, mapendekezo ya kanuni yalijadiliwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya tff na wakakubaliana na hoja za vilabu vya ligi kuu na kupitisha maombi yao.”
Karia aliongeza kupitia wachezaji hao kibiashara itavutia uwekezaji mkubwa kwa makampuni mbalimbali kwasababu Ligi itakuwa na mvuto na ushindani mkubwa.
“Kukiongezeka wachezaji kutoka nje Ligi yetu itakuwa inafatiliwa na mwisho wa siku tutaitangaza na wadhamini wetu watakaonjitokeza watapata fursa pana zaidi ya kujitangaza,”
Karia hakuishia hapo kwani alisema ongezeko hilo la wachezaji litafanya wachezaji kupata nafasi ya kuboresha viwango chao kwa kukutana na wachezaji wenye uwezo lakini pia hata maslahi yao kuwa vizuri.
“Uwepo wa wachezaji wa kigeni utasaidia vijana wetu kujifuza kuwa mpira ni kazi hivyo kuhakikisha wanatunza viwango vyao, kipindi hiki ambacho wachezaji wa kigeni wamekuwa wanasajiliwa imesaidia pia wachezaji wetu kuboreshewa mishahara.”
Msimu wa mwaka 2018/2019.
Kwa msimu huu mpaka tunapoongea wachezaji wa kigeni na vilabu vilivowasajili ni kama ifuatavyo,
1.Simba-8
2.Yanga-2
3.Azam-6
4.Singida-5
5.Biashara-4
6.Stand United-4
7.Mbeya City-1
8. KMC FC-2
Hadi muda huu wachezaji waliombewa wa kigeni ni 32. Ikiwa ni asilimia 5 ya wachezaji watakaosajiliwa.wakati dirisha linafungwa Alhamisi 26 Julia, 2018 kwa idadi iliyopo tunategemea idadi ya wachezaji wa kigeni itapungua tofauti na msimu uliopita tuliokuwa na asilimia 8 ya wachezaji wa kigeni.
Wachezaji wa kigeni waliosajiliwa na vilabu vya ligi kuu lazima watimize masharti ya kikanuni kwa kusajili mchezaji anayecheza timu ya taifa au ligi kuu, au vyote viwili awe mchezaji wa ligi kuu na timu ya taifa.
Kanuni hii imewekwa ili kuwalinda wachezaji wa Tanzania kwa kuwa na wachezaji wenye ubora ambao watasaidia kuboresha viwango vya wachezaji wetu na thamani ya ligi yetu.
Chapisha Maoni