Ajiua kwa kujinyonga kwa mkanda
Mtu mmoja Jabiri Joseph anayekadiriwa kuwa
na umri wa miaka kati ya 25 hadi 30 amekufa
baada ya kujinyonga kwa kutumia mkanda wa
suruali yake.
Kwa mujibu wa polisi, mtu huyo inasadikiwa
alijitundika kwenye nondo ya dirisha la
chumba cha nyumba alimokuwa akiishi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, jijini
Dar es Salaam Camilius Wambura alisema hayo
jana na kuongeza kuwa tukio hilo limetokea
juzi jioni katika Kata ya Mabibo.
Kamanda Wambura alisema polisi walikuta
mwili wa marehemu ukiwa umeketi kitandani
kwake. Hata hivyo alisema kwamba chanzo cha
kifo kinaendelea kuchunguzwa na mwili wa
marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili. Katika hatua nyingine, polisi waliendesha
msako katika maeneo ya Mburahati, Manseze,
Mabibo na Kigogo na kuwakamata
watuhumiwa 50 wakiwa na kete 155 za bangi,
misokoto 50 na pombe haramu ya gongo lita
75.
Watuhumiwa hao ni Juma Shinda (36), Tabaya
Alex (37), Abdi Juma (25), Sudi Idd(33),
Rosemary Mohammed(30), Mariamu Bakari
(50) na wenzao 44.
Aidha katika tukio jingine, Kamanda wa Polisi
mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema
watu 10 wamekamatwa kwa tuhuma za
kukutwa na bangi puri sita pamoja na pombe
haramu ya gongo lita nane.
Watuhumiwa hao ni Laurent Vicent (40), Lisa
Johannes(33), Ali Said(32) na wenzao saba.
Watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani
baada ya upelelezi kukamilika.
Chapisha Maoni