0
Wafuasi wa Chadema jana waliandamana katika mitaa ya Manzese na kusababisha tafrani baada
ya polisi kuwatawanya kwa mabomu ya machozi na risasi.

Maandamano hayo yaliyoanza saa nne asubuhi jana, yalihusisha wanachama takriban 30 kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo la Ubungo.

Yalianzia Manzese Midizini na kuishia Ofisi za Chadema Kata ya Manzese.
Awali, waandamanaji hao waliokuwa na mabango, walikuwa wakikimbia kwa mtindo wa mchakamchaka na kuimba nyimbo za kumdhihaki Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta,
walinuia kwenda katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kuwasilisha malalamiko kuhusu kubadilishwa kwa Rasimu ya Katiba, lakini lengo
lao halikutimia.

Miongoni mwa ujumbe uliobebwa katika mabango hayo ulisema, Sitta, Chenge maoni ya wananchi yaheshimiwe,” “Hatutaki Katiba ya CCM” na
“Hatima ya Tanzania tuitakayo haitapatikana kwa mabomu na vitisho, polisi wetu mtuelewe” ambayo yalikuwa yakiendelea kuandikwa kadiri
walivyoendelea na maandamano.

Baada ya kuzunguka mitaa kadhaa ya Manzese, waandamanaji walifika katika Ofisi za Chadema Kata ya Manzese ambako walikusanyika na kuanza kupeana maelekezo ya namna ya kwenda kwa Mkuu wa Wilaya.

Wakiwa ofisini hapo, Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Kinondoni, Boniface Jacob alisema maandamano hayo ya umbali wa kilometa 3.5 ni sehemu ya maandamano yasiyo na ukomo
yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

“Tumeandamana kwa amani hadi tumefika hapa, hakuna aliyeibiwa wala aliyefanya vurugu. Polisi wametuona, wametuogopa, leo tulikuwa tayari kwa
lolote, hivyo maandamano yetu yanaendelea,” alisema.

Wakati akizungumza hayo na kusisitiza kwamba polisi ndiyo chanzo cha vurugu wanapoingilia na kuwapiga wananchi wanaoandamana kwa amani,
ghafla askari zaidi ya 20 walivamia eneo hilo na kuwatawanya kwa mabomu ya machozi na kupiga risasi hewani.

Katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ambako maandamano hayo yalitarajiwa kuishia, kulikuwa na ulinzi wa polisi waliokuwa wakifanya doria wakati wote.

RPC ayaponda Akizungumzia maandamano hayo, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema hakukuwa na maandamano kwenye mitaa
ya Manzese, bali ni kikundi cha watu wasiozidi watano ambao alidai kuwa ni wahuni.

Wambura alisema watu hao waliotoka
vichochoroni wakiwa wameshika mabango yao na walipowaona askari polisi walikimbia na kuelekea
kwenye mitaa hiyo.
“Mimi sijaona maandamano, wale walioonekana ni wahuni tu ambao hawazidi hata watano waliokuwa
wameshika mabango yao halafu baadaye walipowaona polisi walikimbia kwenye mitaa yao,” alisema Wambura.

Mnyika ataka magereza zaidi
Wakati hayo yakiendelea, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika alisema Serikali iendelee kujenga magereza mengi kwa kuwa
mapambano waliyoyaanza hayatazimika na watakamatwa wengi zaidi.

Akihutubia mamia ya wakazi wa Jiji la Mwanza juzi, Mnyika alisema kamwe hawatishwi kwa kupigwa na kuwekwa magerezani.
Alisema sasa wanaanzisha njia mpya za kufanya maandamano ikiwamo kugoma kufanya jambo lolote, bila kuhitaji kibali cha polisi na maandamano yao hayatasitishwa kwa kupigwa na
kukamatwa.

“Serikali ya CCM ambayo inadhani inaweza kupunguza kasi ya Chadema kwa kutupiga na kutukamata, iongeze kujenga magereza, kwani
yaliyopo hayatoshi tutakwenda wengi huko...” alisema Mnyika.

Chapisha Maoni

 
Top