0
KIPENGA cha kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa, kinatarajiwa kupulizwa Novemba 30 mwaka huu na uchaguzi kufanyika Desemba 14 chini ya
sheria zilizopo.

Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), iliyotumwa katika vyombo vya habari jana, ilifafanua kuwa uchaguzi huo utafanyika kwa kuzingatia masharti ya sheria za serikali za mitaa na kanuni za uchaguzi huo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, sheria hizo zimetungwa na ofisi yake, baada ya kuwashirikisha wadau
mbalimbali wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, asasi za kiraia
na wadau mbalimbali.

Kwa uamuzi huo, wagombea wa nafasi
zinazowaniwa za mwenyekiti wa mtaa, kijiji na kitongoji na nafasi za ujumbe wa serikali za vijiji na kamati za mitaa, wametakiwa wawe wanachama na wadhaminiwe na chama cha siasa
chenye usajili wa kudumu.

Ratiba

Katika ratiba iliyotolewa sambamba na taarifa hiyo, wasimamizi wa uchaguzi wameelekezwa kutoa tangazo la majina na mipaka ya mitaa, vijiji na vitongoji, siku 50 kabla ya siku ya uchaguzi
kwa kuzingatia Kanuni ya 6 ya Kanuni za
Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa ya mwaka
2014.

Baada ya hatua hiyo, wasimamizi hao wa uchaguzi watateua majina ya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi mara baada ya kusambazwa kwa kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa.

Katika eneo lake, msimamizi wa uchaguzi atatoa maelekezo ya uchaguzi siku zisizopungua 28
kabla ya siku ya uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni ya 7(1), 8(1) ya kanuni za uchaguzi wa viongozi
wa mamlaka za serikali za mitaa, ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa za mwaka 2014.

Aidha msimamizi wa uchaguzi atateua ofisa wa umma mwenye sifa na uadilifu, atakayeandikisha na kuandaa orodha ya wapiga kura siku 21 kabla
ya siku ya uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni 8 na 9 ya Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka
za Serikali za Mitaa za mwaka 2014.
Uteuzi wagombea
Baada ya hatua zote hizo za awali kufanyika, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi atabandika orodha ya wapiga kura mahali pa matangazo ya
uchaguzi na kutunza kumbukumbu zake, baada ya kusambazwa kwa kanuni za uchaguzi na kufanya uteuzi wa wagombea siku zisizopungua
20 kabla ya siku ya uchaguzi.
Ratiba iliyotolewa pia inaonesha kwamba Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, katika muda wa
siku mbili tangu siku ya uteuzi kufanyika,
atasikiliza na kutoa uamuzi katika muda usiozidi siku mbili kwa mapingamizi mbalimbali, kuanzia
siku ya kupokea pingamizi husika.
Aidha kutakuwepo na Kamati ya Rufaa, ambayo wajumbe wake watateuliwa na Katibu Tawala wa Mkoa na katika uteuzi wake, Katibu Tawala atazingatia hali halisi ya watumishi wa umma
walioko katika wilaya husika.

Kamati hiyo ya Rufaa, itateuliwa siku saba kabla ya siku za uteuzi wa wagombea kwa mujibu wa
Kanuni ya 16(4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa za mwaka 2014. Kampeni
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, kampeni za uchaguzi zitafanyika wiki mbili za mwisho kabla ya siku ya
uchaguzi na zitafanyika kwa muda wa siku 14 na zitamalizika siku moja kabla ya siku ya uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa za mwaka 2014.

Ili kufanikisha uchaguzi huo, wananchi
wametakiwa kujiandikisha katika Rejista ya Wapigakura, itakayoandaliwa siku ishirini na moja kabla ya siku ya uchaguzi; na uchaguzi utafanywa
kwa kutumia karatasi maalumu za kupigia kura.

Aidha kura zitapigwa na kutumbukizwa kwenye masanduku ya kupigia kura na kama kawaida, uchaguzi utafanyika katika ngazi ya kitongoji na
mitaa katika sehemu ya faragha na hakutakuwa na
mikutano ya uchaguzi katika ngazi za vijiji.

Uchaguzi uliopita Katika uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa,
CCM kilipata ushindi wa kishindo wa zaidi ya asilimia 90 ya kura zote zilizopigwa, hatua iliyochukuliwa na wachambuzi wengi kuwa ni
dalili kuwa chama hicho kilikuwa kinakwenda kushinda Uchaguzi Mkuu wa 2010. Uchaguzi wa mwaka huu, mbali na kuendelea kutumika kutoa ishara za uchaguzi mkuu ujao, pia
utakuwa na umuhimu wa ziada katika kupima uimara wa makubaliano ya vyama vikubwa vya siasa, vilivyounda kundi la Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), wakati wa mchakato wa Katiba mpya na kukubalika kwao kwa wananchi.

Tayari viongozi wa vyama hivyo, Chadema, CUF na NCCR Mageuzi, walishatoa kauli ya kuhoji kwa
nini uchaguzi huo unachelewa, wakihofia kuwepo
wanachoita mchezo mchafu wa kuwashitukiza. Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe, alinukuliwa akidai Serikali imeshindwa
kutangaza tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo, lakini pamoja na hitilafu hiyo, chama hicho kimeshatoa taarifa kwa wanachama wake
kujiandaa kugombea.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya, alinukuliwa akidai kwa kuwa uchaguzi huo hufanyika Septemba kila mara na kwa kuwa
mwaka huu kuna Bunge Maalumu la Katiba linalomalizika Oktoba, Serikali ilitakiwa kulitambua
hilo na kutoa ratiba mapema.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Chadema, John Mnyika alisema kutokana na mchakato wa kupata Katiba mpya kusuasua,
vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
vinatakiwa kushirikiana ili kushinda viti vingi.

Chapisha Maoni

 
Top