ZAIDI ya waathirika 1,000 milipuko ya mabomu Mbagala, wameomba Serikali kuingilia kati na kuwasaidia, ili wapate fidia inayostahili kutokana
na mali na vitu vyao vilivyoharibiwa wakati wa mlipuko huo Aprili 2009.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana mbele ya baadhi ya waathirika hao,
Katibu wa Kamati ya Waathirika hao, Thomas Mbasha, alisema baada ya ajali hiyo, walilipwa fidia ndogo na waliandika malalamiko yao kwa
njia ya maandishi kwa Serikali wakitaka
kuongezwa fidia, lakini hawajapata majibu mazuri.
“Tumeandika barua kadhaa kwa Serikali tukiomba fidia zetu lakini hakuna kilichofanyika. Tunahitaji
Rais aingilie kati suala hili ili tulipwe stahili zetu kabla hajaondoka madarakani,” alisema.
Mbasha alisema fidia walizolipwa awali,
hazikulingana na thamani ya mali na vitu
walivyopoteza wakati wa mabomu hayo.
“Inakatisha tamaa kusema haya mbele ya umma lakini ndicho tulichopewa na Sserikali kama fidia,”
alisema huku akionesha nakala za hundi zikiwa na kiasi walicholipwa.
Baadhi ya hundi za malipo hayo kutoka Benki Kuu (BoT) zilikuwa za Sh 1,400; Sh 2,700; Sh 1,950 na Sh 4,900.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Stephen Gimonge alisema Rais Kikwete alitembelea eneo hilo na
kuahidi kuhakikisha waathirika wanalipwa fidia
inayostahili lakini ahadi hiyo haijazaa matunda.
Wakizungumza na waandishi wa habari, waathirika hao waliokuwa wamekusanyika katika viwanja vya
Shule ya Msingi Mbagala Kuu, wilayani Temeke walithibitisha kupokea hundi zenye kiasi kidogo cha malipo ya fidia, huku wengine wakiandikiwa kulipwa Sh 1,000.
Omary Mbonde ambaye ni mmoja wa waathirika hao, alithibitisha kulipwa hundi ya fidia ya Sh
1,950. “Fedha hizo nimelipwa kama fidia kwa ajili ya nyumba yangu iliyoharibika pamoja na vitu vyangu vingine,” alisema na kuongeza kuwa alipeleka malalamiko yake kwenye kamati, ili apate fidia inayostahili lakini hadi leo hajapata
chochote.
Chapisha Maoni