Mwili wa Salome Richard (17) aliyefariki dunia katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza akidaiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa ebola ulizikwa juzi katika makaburi ya
misheni mjini hapa chini ya uangalizi maalumu.
Mgonjwa huyo alifariki dunia Ijumaa saa 2 usiku baada ya kufika hospitalini hapo akiwa na homa kali. Vile vile madaktari waliokuwa wanatoa huduma kwa mgonjwa huyo wamewekwa kwenye
chumba maalumu kwa ajili ya uangalizi wakati uongozi wa hospitali hiyo ukisubiri majibu ya sampuli kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii.
Hata hivyo, uongozi wa hospitali hiyo ulisema hakuna mgonjwa aliyefariki dunia kwa ugonjwa wa ebola na kwamba mgonjwa huyo aliyetoka katika
eneo la Nyehunge, alikuwa akisumbuliwa na homa
kali.
Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Mary Jose alisema Salome alifikishwa hospitalini hapo Ijumaa saa 4:30 asubuhi akiwa na homa kali.
Alisema muda mfupi baadaye alianza kutokwa na damu puani, mdomoni na sehemu ya haja kubwa,
ndipo aliwekwa katika chumba maalumu kwa uangalizi wa madaktari watatu.
“Jana (Juzi) tulichukua sampuli na kuzipeleka Dar es Salaam Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
kwa uchunguzi zaidi, lakini hatuwezi kusema kwamba ana ugonjwa wa ebola hadi majibu yatakapokuja, tuliamua kuchukua tahadhari.
Tulimlaza kwenye chumba maalumu ili kumfanyia.uchunguzi wa kina,” alisema Dk Jose.
Wakati jana uongozi wa Wizara ya Afya
haukupatikana kwa simu kuzungumzia ugonjwa huo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza imeahidi kutoa tamko leo kuhusiana na kifo hicho.
Mwezi uliopita mgonjwa mwenye dalili kama hizo aliwahi kupatikana katika Hospitali ya Wilaya ya Geita, ambaye baada ya wiki moja alifariki dunia
na majibu ya vipimo vyake yalionyesha kwamba alifariki kutokana na ugonjwa wa chikungunya.
Chapisha Maoni