0
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kutekeleza ahadi aliyoitoa katika Uchaguzi Mkuu 2010 wa kupatikana Wilaya mpya
ya Ulyankulu, mkoani Tabora kabla ya kumaliza kipindi chake cha uongozi mwaka 2015.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara, Bi. Magdalena Sakaya, aliyasema hayo jana katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji
King'wangoko, Kata ya Sasu, Wilaya ya Kaliua, mkoani humo.

Alisema Rais Kikwete alitoa ahadi hiyo wakati akiomba kura kwa wananchi ambapo hivi sasa anakaribia kumaliza kipindi chake cha miaka 10
bila kutekeleza ahadi hiyo hivyo wananchi wanataka kujua hatima yao.

“CUF tutahakikisha Wilaya mpya inapatikana, inashangaza kusikia karibu kata zote za Wilaya ya Kaliua ni sehemu ya hifadhi wakati hakuna miti
wala wanyama wanaoishi maeneo hayo.
“Wananchi wanaendelea na ujenzi wa makazi na vitega uchumi na Mji unaendelea kukua lakini cha kushangaza ramani inaonesha eneo kubwa la Wilaya hii ni hifadhi,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Bw. Abdul Kambaya, alisema anasikitishwa na umasikini uliokithiri kwa
wakazi wa Kaliua licha ya eneo hilo kuwa na madini mengi.

“Mbunge wenu anapokea fedha za maendeleo kila mwezi lakini bado ameshindwa kuwaletea maendeleo hata kujenga barabara kwa kiwango
cha lami,” alisema. Wakati huo huo, chama hicho mkoani humo
kimepanga kufanya maandamano makubwa ya kumpokea Bi. Sakaya atakapowasili kwa mara ya
kwanza katika Mkoa huo wakimpongeza kwa kupata cheo hicho na jitihada zake za kuwatetea wananchi wakiwemo wakulima wa tumbaku.

Katibu wa chama hicho ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa, Kapasha Kapasha,
aliyasema hayo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Lombe, Kata ya Kumbiziganga, Wilaya ya Kaliua, mkoani humo.

Alisema chama hicho kimeweka historia nchini kwa kumchagua mwanamke katika uongozi wa juu tofauti na vyama vingine vya siasa hivyo watampokea kishujaa kwa kufanya maandamano
akitokea Wilaya ya Kaliua.

Chapisha Maoni

 
Top