0
VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uwazi si kutoa maamuzi yanayopendelea kundi moja kwenye
masuala mbalimbali ya chama kwani wakifanya hivyo, watasababisha makundi ambayo yatajengeana chuki miongoni mwa wana CCM wenyewe.

Katibu wa chama hicho mkoani humo, Bw. Deogratius Rutta, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya chama
cha hicho wilayani Mwanga.
Kikao hicho kilipokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho kipindi cha Januari-Desemba
2013, Januari hadi Juni mwaka huu.
Alisema ni vyema viongozi wakawa makini na maamuzi wanayotoa ili wasiwe chanzo cha makundi ndani ya chama hasa kipindi hiki cha
kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu 2015.

"Naomba tusiwatishe na kuwafanya maadui wanachama wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, lazima viongozi tuwe waadilifu,
tusitengeneze makundi na kutoa maamuzi yanayojenga chuki," alisema.
Katika hatua nyingine, Bw. Rutta aliwataka wanachama wa chama hicho na wananchi kwa ujumla, kuwakosoa viongozi wanakosea ili waweze kujirekebisha na kutekeleza majukumu
yao vizuri.

Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Bw. Mathewa Msofe, aliwataka viongozi wa chama hicho kutokuwa vikwazo kwa watu wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na
kuacha kuwabeba baadhi ya wagombea kwa maslahi binafsi.

Alisema ni vyema wakaepuka vitendo vya rushwa ili chama hicho kiweze kupata viongozi bora katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na
Uchaguzi Mkuu ujao.
"Tuanze kujipanga sasa kwa ajili ya chaguzi zijazo, nawaomba tusibweteke, tukipoteza kitongoji au kijiji kimoja, mtu wa kwanza kuwajibika na kulaumiwa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu.

"Wakati mwingine tunaanguka katika uchaguzi kwa sababu ya ubinafsi na rushwa, tuwe makini ili tuweze kuibuka na ushindi wa kishindo katika
chaguzi zilizo mbele yetu," alisema.

Chapisha Maoni

 
Top