GHANA imelazimishwa sare ya 1-1 na Guinea katika mechi ya Kundi E kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco.
Nahodha Asamoah Gyan aliwafungia Black Stars kipindi cha kwanza dakika ya 27 kabla ya Ibrahim Traore kuisawazishia Guinea dakika ya 81.
Ghana inabaki kileleni mwa Kundi E kwa
kufikisha pointi tano, wakati Uganda
iliyofungwa na Togo nyumbani mjini Kampala jana, inabaki na pointi zake nne.
Bao lililoizamisha Uganda jioni ya jana

lilifungwa na Donou Kokou dakika ya 30 na matokeo hayo yanaifanya Togo ibebe pointi tatu za kwanza baada ya awali kupoteza mechi mbili, wakati
Cranes inabaki na pointi zake nne.
Katika mechi nyingine za jana kufuzu AFCON.ya mwakani Morocco, Gabon iliilaza 2-0 Burkina Faso, mabao ya Pierre-Emerick Aubameyang dakika ya 67 na 74 mjini Libreville, Sudan iliwafunga mabingwa watetezi, Nigeria 1-0, bao pekee la Bakri Abd Elgadir dakika ya 41.
Niger ilitoka sare ya 0-0 na Zambia, Kongo ilifungwa 2-0 nyumbani na Afrika Kusini, mabao ya Bongani Ndulula dakika ya 52 na Tokelo Anthony Rantie dakika ya 55, wakati
DRC imefungwa 2-1 nyumbani na Ivory
Coast. Bao la DRC lilifungwa na Cedric
Mongongu dakika ya 71, wakati mabao ya Tembo yalifungwa na Wilfred Bony dakika ya 23 na Max Gradel dakika ya 83.
Msumbiji iliwafunga 2-0 Cape Verde, mabao ya Saddan Guambe dakika ya 43 na Artur Faife dakika ya 60, wakati Sierra Leone imetoka sare 0-0 na Cameroon na Ethiopia ilifungwa 2-0 nyumbani na Mali mabao ya Abdoulay Diaby dakika ya 33 na Sambou Yatabare dakika ya 60.
Malawi ilifungwa 2-0 nyumbani na Algeria mabao ya Rafik Halliche dakika ya 10 nabSaphir Taider dakika ya 93. Katika mechi za juzi Senegal ilitoka 0-0 na Tunisia sawa na Lesotho na Angola, wakati Botswana ilifungwa 2-0 nyumbani na Misri mabao ya
Mohamed El Nenny dakika ya 56 na
Mohamed Salah dakika ya 61. Mechi za
marudiano zitachezwa Jumatano zikiwa ni za kwanza katika mzunguko wa pili.
Chapisha Maoni