(NEC), wakiwa katika kikao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa White
House mjini Dodoma juzi na kuongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya
Kikwete.
Baadhi ya makada wa wa CCM
wanaotajwa kuwania urais kupitia chama hicho wanadaiwa kugeuza mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec), kuwa sehemu ya kampeni kwa wajumbe wabmkutano huo wakidaiwa kumwaga fedha usiku kucha.
Gazeti hili lilishuhudia kampeni hizo
zikifanywa na wapambe wa wagombea
hao nje ya Ukumbi wa Nec uliopo nje ya
jengo la White House mjini Dodoma na
baadhi ya watu wanaotajwa kuwania
nafasi hiyo.
Wapambe hao kwa siku mbili za vikao
vya Nec vilivyofanyika mjini hapa
kuanzia juzi walionekana wakifika
mapema, kusalimia, kujitenga katika
makundi madogomadogo na wajumbe
wa Nec tofauti na vikao vingine
vilivyotangulia.
Harakati hizo hazikuishia katika viwanja
hivyo, bali hata nje ambapo mmoja wa
makada anayetajwa kuwania nafasi hiyo
kutoka Kanda ya Ziwa ameonekana
kukutana na makatibu wa CCM katika
moja ya hoteli mjini hapa.
“Huyu jamaa amekutana na makatibu wa CCM mara nyingi katika kile
kinachoelezwa kuwa ni kusaka wajumbe
ili wasijiunge na kambi nyingine,”
kilieleza chanzo chetu.
Alipoulizwa Katibu wa Itikadi na Uenezi
wa CCM, Nape Nnauye, alisema bado
hajazipata taarifa hizo na kwamba kama
kuna vitendo vya rushwa vinafanyika ni
nje ya mazingira hayo.
Alisema katika mazingira kunapofanyika
kikao cha Nec, si rahisi kuwapo vitendo
hivyo. “Sasa kama wanapeana barabarani mimi itakuwa ni vigumu sana. Mimi ninashughulikia na mambo ya humu ndani (kikao cha Nec),”alisema na kuongeza:
“Leteni taarifa nilikuta fulani anagawa
ama fulani anapokea, haya maneno ya
jumla hivi yanaweza kuwa ni mkakati wa
kupaka chama matope,” alisema.
Alisema kama inagawiwa usiku wakati
yeye akiwa amelala hawezi kufahamu.
Makatibu na wenyeviti wa CCM wa
wilaya wanaingia katika Nec kwa mujibu
wa vyeo vyao.
Tayari hali hiyo imelalamikiwa na baadhi
ya wajumbe wa Nec, wakisema inakitia
aibu chama.
Mmoja wa wajumbe wa Nec, Juma
Kilimbah, alisema kitendo cha kufanya
kampeni ya kutaka kuungwa mkono ni
kinyume cha maadili ya chama.
“Mimi sijafuatwa lakini kama kuna watu
wanafanya kampeni ya kutaka kuungwa
mkono wakati chama hakijatangaza
kuanza kwa mchakato ni kinyume cha
maadili ya chama,” alisema.
Rushwa hiyo inadaiwa kufanywa na
waratibu wa kundi moja linalomuunga
mkono mmoja wa vigogo nchini, ambaye
anatajwa kuwania nafasi hiyo katika
uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.
Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili
umebaini kumekuwa na waratibu kutoka
kanda mbalimbali ambao waligawanywa
katika makundi manne na walikuwa
wakitoa fedha kwa baadhi ya wajumbe
wa Nec ili wamuunge mkono ‘mgombea’
huyo.
Rushwa hiyo imekuwa ikitolewa kwa
usiri mkubwa na mmoja wa viongozi wa
chama hicho ambaye aliwahi kufanya
kazi mkoani Dar es Salaam, anaelezwa
kuwajibika katika kuwapeleka wajumbe
wa Nec ili wakalipwe kwa mmoja wa
waratibu wa mpango huo ambaye
imedaiwa ni mmoja wa mawaziri.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, wajumbe
hao walikuwa wakipewa shilingi milioni
moja kama ushawishi ili wamuunge
mkono ‘mgombea’ huyo.
Hata hivyo, habari za kutolewa kwa
rushwa hizo zilivuja mara baada ya
mmoja wa waratibu wa mpango huo
kutoka kanda ya Nyanda za Juu Kusini
kuwapa wajumbe Sh700,000 badala ya
shilingi milioni moja, jambo ambalo
liliwachefua wajumbe waliopunjwa
mgawo huo.
Wajumbe waliolengwa zaidi ni wale
walioonyesha nia ya kuhamia kwenye
kundi la mgombea mwingine,
anayeonekana kuwa na nguvu zaidi ya
wenzake.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, kampeni
za kutafuta wajumbe wa Nec
wanaowaunga mkono, zinalenga katika
mmoja wa watu wanaotajwa kuwania
urais kuwa na uhakika wa kupata kura
zaidi 190 kati ya wajumbe 370 wa Nec.
Akizungumza kwa njia ya simu kuhusu
madai hayo, Mkuu wa Taasisi ya
Kudhibiti na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) wa Mkoa wa Dodoma, Emma
Kuhanga, alisema hawajapokea madai
yao.
Hata hivyo, aliahidi kufanyia kazi taarifa
alizozipata kutoka kwa mwandishi wa
habari.
“Hatujapata madai hayo lakini kutokana
na swali lako tunalichukulia kama taarifa
ya kuanza kufanyia kazi,” alisema.
WanaCCM ambao wamekuwa wakitajwa
kuwania urais ni Waziri Mkuu Mizengo
Pinda, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira,
Waziri Mkuu wa zamani Edward
Lowassa na mtangulizi wake katika
nafasi hiyo, Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Kazi Maalumu), Profesa Mark
Mwandosya, Mbunge wa Songea Mjini,
Dk Emmanuel Nchimbi na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine ni Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Samuel Sitta. Wengine
wanaotajwa ni Waziri wa Uchukuzi, Dk
Harrison Mwakyembe, Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa
Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro.
Pia wamo Waziri wa Maliasili na Utalii,
Lazaro Nyalandu na Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,
January Makamba.
Tayari CCM imeshawafungia kufanya
kampeni baadhi ya makada wake
walioonekana kuanza kufanya kampeni
kabla ya muda.
Waliotangazwa kufungiwa na kuwekwa
chini ya uangalizi ni Lowassa, Membe,
Makamba, Ngeleja, Wasira na Sumaye.
Na Mwananchi
Chapisha Maoni