MWANDAAJI wa mashindano ya urembo Tanzania, Miss Tanzania, Hashim Ludenga amewasilisha pingamizi la awali katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akipinga kuzuiwa kuendelea kuendesha mashindano hayo yanayotarajiwa kufikia kilele chake Oktoba 11, mwaka huu.
Lundenga kupitia kwa Wakili Audax Kahendaguza, aliwasilisha pingamizi hilo dhidi ya ombi la kuzuiwa kuendelea kuendesha mashindano hayo
lililofunguliwa na mwanzilishi mwenzake wa mashindano hayo, Prashant Patel.
Katika pingamizi lake, Lundenga amewasilisha hoja nne akidai mahakama hiyo haina mamlaka
ya kutoa amri iliyoombwa na Patel.
Patel aliwasilisha ombi chini ya hati ya dharura, kupitia kwa wakili wake Benjamin Mwakagamba, akidai Lundenga ana mpango wa kuendesha
mashindano hayo kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, kinyume cha sheria na bila hata kumtaarifu.
Anaomba mahakama itoe zuio dhidi ya mshirika wake, Lundenga, kuendesha mashindano hayo hadi shauri lake la msingi aliloliwasilisha litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Wakili Mwakagamba aliiomba mahakama isikilize ombi pamoja na pingamizi kwa pamoja.
Hakimu Mkazi Frank Moshi alikubali ombi hilo na kuahirisha shauri hilo hadi leo asubuhi kwa ajili ya kusikiliza ombi pamoja na pingamizi lililowasilishwa na Lundenga.
Katika kesi ya msingi, Patel anadai pamoja na mambo mengine, utekelezaji wa makubaliano ya Februari 20, 2012 na malipo ya Sh milioni 19 ambayo hayajalipwa kwa mujibu wa mkataba na
faida nyinginezo ambazo zimejitokeza hadi Septemba 23, mwaka huu.
Katika hati ya kiapo inayounga mkono ombi hilo, Patel anadai kuwa yeye pamoja na Lundenga, ndiyo waanzilishi, waongozaji na waendeshaji wa
mashindano ya Miss Tanzania na wamekuwa katika hali hiyo kwa miaka 20 sasa, tangu mashindano hayo yaliyoporuhusiwa tena mwaka
1994.
Kwa kipindi chote hicho, wamekuwa wakisaini makubaliano ya namna ya kuendesha mashindano hayo na mara ya mwisho walisaini makubaliano
Februari 20, 2012.
Hata hivyo, Lundenga alikataa kusaini
makubaliano kwa mwaka 2013 na 2014 na ameshindwa kumlipa fedha zake Sh milioni 19 badala yake Ludenga ameshirikiana na wadhamini
wengine kuendesha mashindano hayo.
Kwa mujibu wa makubaliano, Lundenga pia alipaswa kulipa pauni za Uingereza 30,000 kama malipo ya kibali kwa mwendeshaji wa shindano
hilo duniani, Miss World, deni ambalo limekuwa la muda mrefu, hivyo kuchafua hadhi yake.
Patel anadai kuwa Ludenga alipelekewa taarifa na wakili wake kulimaliza suala hili bila kushirikisha hatua za kisheria, lakini alikaidi.
Hivyo Patel anadai kuwa hakuwa na njia nyingine zaidi ya kulipeleka suala hilo mahakamani.
Chapisha Maoni