0
Ni msemo maarufu wa wahenga ambapo Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein aliutumia
vilivyo juzi katika hotuba yake baada ya yeye na
Rais Jakaya Kikwete kupokea Katiba
Inayopendekezwa kutoka kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba (BMK), Samuel Sitta
mjini Dodoma.
Alisema: ‘Hayawi hayawi sasa yamekuwa’ na akaendelea zaidi kwa kusema: ‘Waliosema
hayawezekani sasa yamewezekana’.
Ni maneno ya kiongozi wa ngazi ya juu katika taifa letu na pia ndiyo maneno ya viongozi wengine na wananchi wapenda amani katika nchi ya Tanzania baada ya kupatikana kwa Katiba
Inayopendekezwa na kukabidhiwa rasmi kwa viongozi hao wakuu wa nchi kama ilivyokusudiwa
kwa sheria na taratibu.

Katika hotuba yake kwenye tukio hilo la kihistoria, Rais Kikwete alitamka wazi tena kwa furaha kwamba Katiba Inayopendekwezwa imeandaliwa
kwa ubora wa hali ya juu na kusema kuwa kwa kupatikana katiba inayopendekezwa ajenda ya
Watanzania imetimia.

Mapema Mwenyekiti Kamati ya Uandishi, Andrew
Chenge aliweka bayana katika sherehe hiyo kwamba asilimia zipatazo 82 ya mambo yaliyokuwemo katika rasimu ya Katiba iliyokabidhiwa BMK na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji mstaafu Joseph Warioba
yameingizwa katika Katiba Inayopendekezwa na
asilimia zipatazo 18 tu ndiyo mambo mapya yaliyofanyiwa marekebisho na wajumbe. Kwa kiwango chochote kile cha ufaulu duniani, hiki ni kiwango cha hali ya juu na kinastahiki
kupongezwa na kila mpenda haki na maendeleo mema ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni. Ndani ya Katiba Inayopendekezwa makundi maalumu yakiwemo walemavu, vijana,
wanawake, wafugaji, wavuvi, wachimba madini na mengineyo, yamepewa umuhimu unastahili.

Tuna kila sababu ya kuwapongeza wabunge wote wa BMK waliweza kufikia hatua hiyo muhimu na ya ngazi ya juu katika mchakato mzima wa
kutunga katiba mpya ya nchi.
Ni ukweli kwamba kuna changamoto nyingi zilizopitiwa hadi kufikia ngazi hii, lakini yote ni sehemu tu ya mchakato mzima wa kupatikana kwa katiba nzuri yenye mshiko na maslahi ya
taifa.

Kwa hatua hii tuliyofikia, tunapenda kuwashauri Watanzania wote kwamba sasa ni vema kusahau
tofauti zilizokuwapo wakati wa mchakato uliopita
ili kusonga mbele katika hatua itakayofuata ya kuipigia kura ya ndiyo au hapana, kwa mujibu wa
sheria na taratibu zilizopo.

Hapa tunapenda kuchukua usemi aliotumia Msanii Mrisho Mpoto juzi wakati anatumbuiza katika
sherehe hizo, kwamba ‘Palipoacha kuwasha usipakune tena.’ Kwa hali ya kawaida kabisa maana yake ni kwamba: ‘Yaliyopita si ndwele,
tugange yajayo.’ Huu sasa ni wakati wa Watanzania kushikamana
kwa hali na mali licha ya tofauti zilizopo,
kuhakikisha kwamba wakati wa kupiga kura ya Katiba Inayopendekezwa, wanashiriki kwa amani, upendo, mshikamano na umoja kama ilivyo mila
na desturi. Mungu ibariki Tanzania.

Chapisha Maoni

 
Top