SHERIA iliyopitishwa na wakazi wa Arumeru mkoani Arusha ya kuwachapa viboko 70 hadi 120 wasichana wanaovaa nusu uchi na wavulana
wanaovaa mlegezo, kuvuta bangi, wizi, matusi na ulevi nyakati za kazi imeanza kufanya kazi baada ya kijana Zakayo Leonard (26) kuchapwa viboko
120 kwa makosa mbalimbali likiwemo uchafu wa kutofua nguo zake.
Kijana huyo mkazi wa Ilboru, alihukumiwa adhabu hiyo kwa kuchapwa viboko 70 akidaiwa kutenda
kosa la kumshambulia baba yake mzazi
aliyetambulika kwa jina la mzee Ng’uraa na kumng’oa jino moja.
Pia alitandikwa viboko 30 kwa kosa la kumtolea maneno machafu mzee wa kimila (Laigwanani) na baadaye alicharazwa viboko 20 kutokana na tabia
ya uchafu wa kutofua nguo zake.
Hata hivyo, mara baada ya adhabu hiyo ya viboko 120 kwa mkupuo, kijana huyo alizimia na kushindwa kuinuka wala kutembea hali iliyolazimika kusaidiwa kwa kubebwa na morani wa Kimasai hadi nyumbani kwake.
Adhabu hiyo ilitekelezwa hadharani mbele ya wazee wawili wa ukoo (Laigwanani) waliokuwa
wakishuhudia huku mtuhumiwa akitakiwa kutojigusa popote wakati wa utekelezaji wa adhabu hiyo na kwamba iwapo angejishika popote
viboko hivyo alivyochapwa vingefutwa na kurejea upya.
Wazee wa makabila ya Wamasi, Waarusha na Wameru wamejiwekea utaratibu wa kimila bila
kujali kama unafuata maadili ya mwanadamu kwa kuwaadhibu wahalifu hadharani bila kuwafikisha
kwenye vyombo vya sheria.
Chapisha Maoni