0
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini Mhe. Zitto Kabwe, ameibuka mwanasiasa wa kwanza barani Afrika
kutwaa Tuzo ya Mtetezi wa Haki ya Hifadhi ya Jamii, imefahamika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mwishoni mwa wiki na Umoja wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya Nchi za Afrika Mashariki na Kati (ECASSA)
Mhe. Zitto anatarajiwa kukabidhiwa tuzo yake hiyo katika sherehe rasmi iliyopangwa kufanyika
Oktoba 30 na 31 mwaka huu katika mji wa Livingstone nchini Zambia.

“Tuzo hii imetolewa kwako kwa kuzingatia mchango wako mkubwa unaoutoa kuhakikisha
sehemu kubwa ya Watanzania ambao walikuwa hawanufaiki na mifuko hii wanafaidika nayo.
“ECASSA, mahususi kabisa, imevutiwa sana na jitihada zako za kuhakikisha kwamba wasanii wananufaika na mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja
na wakulima kupitia chama chao cha ushirika cha Rumako kilichopo Kigoma Vijijini,” ilisema sehemu ya barua ya umoja huo kwa Zitto
RUMAKO ni Ushirika wa Msingi wa Vijiji vya Mkabogo, Rusaba na Matyazo wilayani Kigoma Vijijini ambako zaidi ya wakulima wake 750 wameingia kuwa wanachama wa Mfuko wa Taifa
wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Kwa takribani miaka minne sasa, Zitto amekuwa akipigania wakulima wa Tanzania kupewa uanachama wa wa mifuko hiyo ili kuwakwamua
kiuchumi na pia kuwawezesha kupata huduma ya hifadhi kama ilivyo kwa wafanyakazi katika sekta
rasmi wanaopata huduma hizo.

Baada ya wakulima hao wa Kigoma, kumekuwepo na wimbi la vyama vingi vya wakulima katika maeneo mbalimbali nchini kutaka kuingia katika
mifuko hiyo na ECASSA inaamini kwamba Zitto ana mchango mkubwa katika hilo.
Akizungumzia tuzo hiyo, Zitto alisema, "
nimeipokea tuzo hii kwa unyenyekevu mkubwa. Naamini kuwa siku za usoni haki ya Hifadhi ya jamii kwa wananchi itakuwa ni haki ya kikatiba.

Nchi masikini zinapaswa kuongeza uwekaji akiba ili ziweze kuendelea kwa kasi. Bila akiba uwekezaji unakuwa mdogo na hatimaye uchumi
haukui.
"Hifadhi ya jamii ni moja ya njia mwafaka kabisa
ya kukuza uwekaji akiba katika nchi kwani wanachama wanafaidika na mafao ya muda mrefu kama pensheni na yale ya muda mfupi kama
Bima ya Afya na mikopo kupitia saccos".
Azimio la kutolewa kwa tuzo hiyo lilitokana na Mkutano Mkuu wa Sita wa ECASSA uliofanyika jijini Kampala, Uganda miaka miwili iliyopita,
ambapo wakuu wa mifuko hiyo walikubaliana iwepo ili kuchochea wanasiasa kuhamasisha
wananchi kuelewa umuhimu wa Hifadhi ya Jamii.
ECASSA ni umoja unaounganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii takribani 20 katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na
Zambia.

Chapisha Maoni

 
Top