Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amefanya mkutano mkubwa Urambo Mashariki na kumshutumu Mbunge wa jimbo hilo, Samuel Sitta
kwa kuchakachua maoni ya wananchi katika mchakato wa Katiba Mpya.
Katika mkutano huo ulifanyika katika Uwanja wa Extended mjini Urambo takriban mita 100 kutokabnyumbani kwa Sitta aliyeongoza Bunge la Katiba,
Mbowe alisema historia ya nchi hii itamhukumu mbunge huyo kwa maovu hayo.
Alisema kutokana na uovu huo wa Sitta ambaye amekuwa akiisifia Katiba Inayopendekezwa kuwa itakuwa nzuri Afrika Mashariki na Kati, vyama vya
upinzani vitaendelea kuidai katiba ya wananchi hata kwa miaka 100 ijayo.
Aprili mwaka huu, wabunge wa vyama vya upinzani chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), walisusia Bunge la Katiba mjini Dodoma wakilalamikia kuvunjwa kwa kanuni na kutofuatwa kwa mapendekezo ya wananchi yaliyotolewa katika Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Akihutubia mamia ya wafuasi wa chama hicho kwenye Operesheni Delete CCM, Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa, alisema ana
uhakika Sitta ataipata hukumu hiyo ya historia kwa kile alichosema kudhulumu haki ya Watanzania milioni 45.
Mbowe anayetumia chopa katika ziara hiyo, alifika katika uwanja huo saa 11.45 na kuhutubia kwa dakika 30.
“Mzee Sitta najua upo nyumbani hapo na unanisikia, kama hunisikii basi mke wako Mama Margreth Sitta atakuwa ananisikia, lakini kama naye hayupo basi kutakuwa na wahudumu
watanisikia na watakuja kukueleza,” alisema huku akiwaonyesha wafuasi wa chama hicho nyumba ya Sitta iliyopo jirani na uwanja huo.
Alisema Sitta alipuuza maoni ya wananchibwaliyotoa katika mchakato wa Katiba Mpya na ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba badala yake
akaweka maoni ya chama chake cha CCM.
“Tunasema kwamba historia ya nchi hii
itamhukumu kwa maovu aliyoyafanya kukataa maoni ya wananchi na kuweka maoni ya chama chake,” alisema.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, alisema baada ya maoni ya wananchi kuchakachuliwa...
“Sasa tutaidai Katiba Mpya hata kwa miaka 100 ijayo.”
Alisema wabunge wa vyama vya upinzani walimwamini Sitta kwa kumpigia debe na baadaye
walimpa kura iliyomfanya awe Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba kutokana na rekodi yake
alipokuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
“Tulifanya hivyo kwa kumwamini kutokana na rekodi zake akiwa spika, tunajuta kumchaguabhatukufahamu kwamba atatusaliti na kudhulumu
haki za Watanzania,” alisema Mbowe.
Hivi karibuni Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi alilieleza gazetin hili katika mahojiano maalumu kuwa Sitta aliwageuka wapinzani baada ya kuwaomba wamchague kuwa
mwenyekiti akiahidi kupigania serikali tatu, lakini baada ya kupata nafasi hiyo akapigania serikali mbili, madai ambayo Sitta aliyapuuza akisema Sugu hakuwa saizi yake.
Mbowe alisema Sitta ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alidiriki kuwatukana hata viongozi wa dini waliomshauri
kuhusu umuhimu wa maoni ya wananchi katika Katiba.
Wakati wa Bunge la Katiba linakaribia ukingoni Septemba mwaka huu, Sitta alitumia maneno makali kuwajibu viongozi wa dini waliotoa waraka
kukosoa mwenendo wa Bunge hilo, akisema waraka huo ulikuwa wa kipuuzi na haukuwa na utukufu wa Mungu.
Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrobazi Katambi alisema kwa heshima ya wananchi wa Mkoa wa Tabora,
Sitta (72), anatakiwa kupumzishwa katika nafasi zake zote za uongozi kutokana na umri wake.b“Ni kweli mzigo mzito anatakiwa kubebeshwa
Mnyamwezi lakini kwa umri alionao Sitta ni kama tunamkosea adabu kwani huu ni muda wake wa kupumzika, tusimchague tena,” alisema huku
akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.
Ufisadi bomba la gesi
Mbowe alitumia mkutano huo kuitaka Serikali kuitisha wakaguzi wa kimataifa ili wachunguze mkataba wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ambao alidai kuna
ufisadi wa Sh1.2 trilioni, vinginevyo atawaeleza wananchi ili waamue.
Juzi, Mbowe aliwatuhumu vigogo wa Serikali kuwa waliongeza fedha katika mradi huo ambazo waligawana kwa masilahi yao binafsi lakini mkopo
huo kutoka China utalipwa na Watanzania wote.
Alisema mradi huo ulikuwa wa Sh1.2 trilioni lakini vigogo hao waliongeza kiasi kama hicho na kugharimu Sh2.4 trilioni.
Alisema ukaguzi unatakiwa kufanyika ili kufahamu thamani ya fedha halisi zinazotakiwa kujenga bomba hilo na fedha zilizotolewa na Serikali.
“Hili nitalisema popote bila woga na niko tayari kukamatwa lakini sitakaa kimya nikishuhudia Watanzania wakilipa deni la fedha walizogawana vigogo hao,” alisema Mbowe.
Alisema ikiwa Serikali ina nia ya dhati kupambana na ufisadi, iweke hadharani mkataba wa ujenzi wa bomba hilo... “Ndiyo maana mikataba hiibimekuwa siri, inafichwa ili wananchi wasiione
lakini tunasema Chadema tutaendelea kuipata na mafisadi watajulikana.”
Chapisha Maoni