0
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) inatarajia kuwahoji Mwanasheria Mkuu (AG), Jaji Frederick Werema, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Robert Mboma na wengine waliotajwa katika kashfa ya kuchotwa Sh. bilioni 306 ya akaunti ya Tegeta
Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Hatua hiyo imekuja baada ya kamati hiyo kukabidhiwa ripoti ya ukaguzi wa hesabu za akaunti hiyo na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai jana ili kuifanyia uchambuzi na kutoa mapendekezo.

Ukaguzi wa hesabu na uchunguzi huo vilifanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru).

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alimkabidhi Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, ripoti hizo, katika Ofisi za Bunge, mjini hapa Dodoma.Waliokuwapo katika makabidhiano hayo ni Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe
na wajumbe wa kamati hiyo; Ally Keissy (Nkasi Kaskazini-CCM), Kombo Khamis Kombo (Mgogoni-CUF) na Ismail Aden Rage (Tabora Mjini-CCM).

Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah.Akikabidhi ripoti hiyo, Ndugai aliitaka PAC kuifanyia uchambuzi na kutoa mapendekezo.
Hata hivyo, aliitaka ihakikishe inajikita katika kutumia ushauri uliotolewa na CAG na Takukuru katika kutoa mapendekezo kwa sababu waliwahoji
wahusika wote.”Baada ya kukamilisha kazi, taarifa irudi kwangu ili kujiridhisha kabla ya kuiwasilisha bungeni,” alisema Ndugai.

Baada ya kupokea ripoti hiyo, Zitto akihojiwa na waandishi wa habari, alisema wa kwanza kuhojiwa
na kamati yake atakuwa ni CAG. Zitto alisema kwamba na kwamba kamati itafanya kazi iliyokabidhiwa na Ofisi ya Spika kwa siri.

Alisema watafanya kazi hiyo kwa siri kwa kuwa ndani ya suala hilo kuna mambo ya mahakama, hivyo wanaepuka kuingia katika malalamiko hapo
baadaye ya mtu kuonewa na kwamba,
watahakikisha wanatenda haki.
Naye Filikunjombe alisema kamati yake ina uwezo mkubwa wa kumaliza kazi hiyo ndani ya siku 10, kuanzia sasa kwa kuwa kazi kubwa imekwisha kufanywa na CAG.

IPTL WANENA
Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) imesema itatoa ushirikiano kwa Bunge pindi watakapohitajika
kufanya hivyo.IPTL ilisema hayo kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Meneja Uhusiano wake, Sylvester Joseph.

"Kwa niaba ya mwenyekiti wa Kampuni za IPTL na PAP, tunaahidi kutoa ushirikiano kwa kamati ili ifanye kazi yake vizuri kama tulivyotoa ushirikiano
tangu uchunguzi ulivyoanza,” ilieleza taarifa hiyo ya IPTL.

Iliongeza: “Tunachoomba ni kwamba, kamati ifanye kazi yake kwa uadilifu ili suala hili liishe na tuweze kujikita sasa katika kuzalisha umeme kwa
ajili ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
"Juzi tulisikia watu wakisema kuwa ripoti imetoka na baadhi ya vyombo vya habari hata kwenye mitandao ya kijamii kuwa ripoti hii imetoka...hatujui wapi ripoti hiyo ilitoka, ila tunataka umma ujue kuwa sasa ndiyo ripoti
imekabidhiwa.”

Kashfa ya Tegeta Escrow iliibuliwa bungeni na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila.Kuibuliwa kwa kashfa hiyo, kulisababisha Kafulila kuingia kwenye malumbano makali yaliyowafikisha katika kutoleana maneno ya
dharau na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, bungeni.

Maneno hayo ya dharau yalihusisha Jaji Werema kumwita Kafulila kuwa ni tumbili na Kafulila kumwita Jaji Werema mwizi.Baadhi ya wabunge wamekuwa wakishinikiza wakitaka ripoti hiyo
pamoja na ile ya uchunguzi uliofanywa na Takukuru ziwasilishwe bungeni ili zikajadiliwe na wabunge ili ukweli ujulikane.

Tayari nchi wahisani zimetangaza kuikatia misaada serikali ya zaidi ya Sh. trilioni 1 kutokana na kashfa hiyo.Akaunti ya Tegeta Escrow
ilifunguliwa kutokana na kutoelewana kuhusu gharama halisi na halali za umeme unaozalishwa na kampuni ya kufua umeme ya IPTL na kuuzwa
Tanesco.

Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID), katika uamuzi wake wa Februari 2014, ilitoa hukumu kuonyesha kwamba Tanesco walitozwa kiwango cha juu zaidi ya kilichopaswa kulipwa
kwa IPTL.

Kwa uamuzi huo, ni dhahiri kwamba fedha zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye akaunti ya Escrow zilipaswa kugawanywa kwa IPTL na
Tanesco baada ya hesabu kufanyiwa marekebisho upya kwa viwango halali, lakini badala yake fedha hizo zilitoweka ghafla kwenye akaunti hiyo.

KILICHOMO KATIKA RIPOTI YA CAG
Matokeo ya ukaguzi uliofanywa na CAG kuhusiana na kuchotwa kwa Sh. bilioni 306 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow yameiweka matatani Ofisi ya
Mwananasheria Mkuu wa Serikali (AG), huku yakizitambua fedha hizo kuwa ni za umma.

Vyanzo vyetu mbalimbali vimebainisha kuwa Ofisi ya AG inadaiwa kuingia matatani, baada ya ripoti ya ukaguzi huo iliyovuja, kubaini kwamba, inahusika moja kwa moja katika kuisababishia
serikali hasara ya jumla ya Sh. bilioni 321 katika kashfa hiyo.

Pia Wizara ya Nishati na Madini, nayo pia inatajwa na ripoti hiyo kuhusika katika kuisababishia serikali hasara hiyo.
Vilevile, Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) nayo pia imeingia matatani, baada ya kuhusishwa na ripoti hiyo kwa tuhuma za kulikosesha shirika hilo kiasi hicho cha fedha.

Ofisi ya AG inahusishwa na kashfa hiyo, baada ya ripoti hiyo kueleza kuwa ilivunja sheria makusudi kwa kuelekeza kuwa Kodi ya Ongezeko la
Thamani (VAT) kwenye gharama za uendeshaji (capacity charges), ambazo Tanesco walilipishwa na IPTL, isilipwe.

Maelekezo hayo ya ofisi ya AG yanadaiwa kusababisha serikali kupoteza mapato ya Sh.
bilioni 21.

Aidha, wizara ya Nishati na Madini inaguswa na taarifa hiyo kwamba ilisaini nyaraka kuidhinisha kutolewa fedha hizo kwenye akaunti hiyo bila kuhakikisha fedha za Tanesco zinarudi.

Hatua hiyo ya wizara hiyo inadaiwa kuipotezea Tanesco kiasi hicho cha fedha. Nayo Bodi Tanesco inaguswa katika kashfa hiyo kwa madai kwamba, haikutimiza wajibu wake kwa kugeuza maamuzi yake na hivyo kulikosesha
shirika kiasi hicho cha fedha.

Ripoti ya CAG inaigusa Bodi hiyo ikisema kwamba iligeuza maamuzi yake ama kwa kushinikizwa na wizara au kwa rushwa.
Ripoti hiyo imebainisha pia kuwa Wizara ya Nishati na Madini haikujiridhisha kuhusu uhalali wa umiliki wa IPTL.
Pia imebaini kuwa Kampuni ya PAP haikununua kihalali asilimia 70 ya hisa za kampuni ya Mechmar katika IPTL kwa madai kwamba, zilizuiwa na mahakama.

Vilevile, imebaini kuwa kampuni hiyo (Mechmar) hawana hati halisi za hisa (share certificates). Ripoti hiyo imebainisha pia kuwa PAP ilifanya
udanganyifu mkubwa katika malipo ya kodi kwa kutoa nyaraka za uongo kuwa walionunua hisa kwa Sh. milioni sita, badala ya Dola za Marekani
milioni 20 na kuikosesha serikali mapato ya Sh. bilioni 8.7.

Inabainisha kuwa fedha zilizokuwamo kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, ambazo ni jumla ya Sh. bilioni 306 ni matokeo ya Tanesco kulipishwa
gharama za uendeshaji zaidi ya kiwango
kinachotakiwa kulipwa. Ripoti hiyo inabainisha kuwa Tanesco walipaswa
kurejeshewa Sh. bilioni 321 zilizolipwa ziada kwa IPTL kati ya mwaka 2002-2012.

Hivyo, fedha za akaunti ya Tegeta Escrow ni fedha za umma na kwamba, yote ilipaswa kurudi Tanesco na shirika kuendelea kuwadai IPTL Sh.
bilioni 15

Chapisha Maoni

 
Top