Mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Mfinzi wilayani Nkasi-Sumbawanga anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kummwagia maji ya moto mumewe na kumsababishia kifo, kisha
kuutumbukiza mwili wake mtoni.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi usiku kijijini hapo na kumtaja aliyeuawa kuwa
ni Evod Teola (62).
Alisema siku ya tukio mwanamume huyo alirejea nyumbani na kuanza mzozo na mkewe aliyemtaja
kwa jina la Zelena Kiozya (55) ambaye alikimbilia jikoni na kuchukua maji ya moto aliyomwagia usoni na tumboni.
Alisema Evod alipata majeraha makubwa na kutokana na kukosekana kwa huduma ya haraka, alifariki dunia usiku huo.
Kamanda Mwaruanda alisema siku iliyofuata, mwanamke huyo akishirikiana na wazazi wake, waliuchukua mwili wa marehemu na kwenda kuutupa kwenye Mto Mfinzi kwa lengo la kupoteza
ushahidi.
Alisema mpaka sasa polisi wanamshikilia mwanamke huyo na wanaendelea kuwasaka wengine waliomsaidia kutaka kupoteza ushahidi.
Watu hao wanadaiwa kutoweka kijijini hapo siku ya tukio.
Kwa mujibu wa Mwaruanda, mwanamke huyo atafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya
polisi kukamilisha uchunguzi wa awali.
Mwaruanda amewaonya wakazi mkoani hapa dhidi ya vitendo vya kujichukulia sheria mkononi ili kuepuka mkono wa dola.
Aliwataka wawe wepesi wa kutafuta suluhu ya matatizo kwa njia ya majadiliano na kwa kushirikisha watu ama vyombo vya sheria viweze
kutafuta suluhisho.
Chapisha Maoni