Ripoti ya ufisadi katika akaunti ya Escrow itawasilishwa bungeni Novemba 27, mwaka huu na kujadiliwa baada ya Kamati ya Uongozi ya Bunge kuridhia kwamba Kamati ya Hesabu za
Serikali (PAC) inaweza kushughulikia suala hilo.
Taarifa zinaeleza kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya baadhi ya wenyeviti wa kamati za Bunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Uongozi kutaka
suala hilo lijadiliwe katika Bunge linaloendelea ili wanaopaswa kuwajibika kutokana na ufisadi huo
wachukuliwe hatua.
Mjumbe mmoja wa kamati ya uongozi ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema jana wamekubaliana kwamba hakuna haja ya kuundwa tume kama ilivyokuwa imeombwa awali na
Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba bali, PAC ambayo ndiyo kamati husika inayoweza kuchunguza suala hilo na kuliwasilisha baada ya
kupata ripoti ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Hata hivyo, Naibu Spika, Job Ndugai ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya uongozi iliyokaa juzi jioni, hakutaka kuzungumzia suala hilo ambalo awali liliibuliwa bungeni na Mbunge wa
Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila akielekeza kuwa ratiba ya shughuli za Bunge ina mwongozo mzima wa nini kitafanyika.
Ratiba hiyo inaonyesha kuwa Novemba 27, PAC itatoa taarifa maalumu bungeni ambayo mwenyekiti wake, Zitto Kabwe alisema inahusu uchunguzi wa Akaunti ya Tegeta Escrow na kwamba Bunge litajadili taarifa hiyo baada ya
kamati kuiwasilisha.
“Ripoti inaweza kuiangusha Serikali kwa Waziri Mkuu kulazimishwa kujiuzulu. Iwapo ripoti ya CAG itaonyesha kuwa suala hilo siyo safi, basi Waziri
Mkuu atatakiwa kujiuzulu kwa kuwa aliwahi kusema suala la Escrow liko sawa,” alisema Zitto.
Suala hilo lilizua mjadala bungeni juzi ambako Ndugai akitoa mwongozo ulioombwa na Kafulila kwamba hoja hiyo kuhusu lini Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda atawasilisha ripoti hiyo baada ya uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambanabna Rushwa (Takukuru) na CAG kukamilika kwa
kuwa ni ya haraka alisema; “Suala la Kafulila
tutalishughulikia kwenye Kamati ya Uongozi kwa kuwa kiti hiki hakina mamlaka.” Baada ya Kafulila kuomba mwongozo huo aliungwa mkono na wabunge wa upinzani na
baadaye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi
alisimama na kusema, “Ni kweli Waziri Mkuu alitoa maelekezo kwa Takukuru na CAG kufanya uchunguzi huo na kukabidhi ripoti kwake ili atoe
taarifa bungeni, lakini kazi hiyo haijakamilika.” Lukuvi alisema ukaguzi wa CAG bado unaendelea
kwa kuwa unahusu mambo mengi na kwamba taarifa zinaeleza kuwa wako mbioni kukamilisha hivyo wakikabidhi kwa waziri mkuu itawasilishwa
bungeni na kukabidhiwa kwa Spika kwa ajili ya utekelezaji.
Alisema taarifa hizo mbili hazijakabidhiwa kwake
na kwamba Takukuru ikimaliza uchunguzi wake inaweza kuchukua hatua yenyewe lakini taarifa
inayosubiriwa na Bunge ni ya CAG.
Chapisha Maoni