0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefanya uteuzi wa Makatibu Wakuu wa Wizara kwa kuteua
Makatibu Wakuu wanne wapya na kuhamisha mmoja.

Aidha, Rais Kikwete amefanya uteuzi na uhamisho wa Makatibu Tawala wa Mikoa. Taarifa iliyotolewa mjini Dodoma jana jioni, Jumatano, Novemba 5, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue imesema kuwa walioteuliwa kuwa Makatibu Wakuu ni Dkt. Donan
Mmbando ambaye anakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Yohana Budeba ambaye anakuwa Katibu Mkuu Wizara ya
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mhandisi Mbogo Futakamba kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji
na Dkt. Adelhelm James Meru ambaye anakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii na Maliasili.

Kabla ya uteuzi wake, Dkt Mmbando alikuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Budeba alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mifugo, Mhandisi Futakamba alikuwa
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji na Dkt. Meru alikuwa Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA).

Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa Rais Kikwete amemhamisha Bibi Maimuna Tarishi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda kuwa Katibu
Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria
Kuhusu uteuzi na uhamisho wa Makatibu Tawala wa Mikoa, Rais Kikwete amemteua Bw. Charles
Pallangyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Bw. Adoh Steven Mapunda, Mkurugenzi
Mtendaji, Manispaa ya Bukoba kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Bw. Severine Kahitwa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro na Dkt.

Faisal Issa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza. Wakati huo huo, Rais Kikwete amemteua Kanali (Mst) Joseph Simbakalia, Mkuu wa Mkoa wa
Mtwara, kuwa Mkurugenzi Mkuu wa EPZA.

Uteuzi huo umeanza jana na Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa wataapishwa leo, Alhamisi, Novemba 6, 2014, Ikulu, Dar es Salaam.

Chapisha Maoni

 
Top