0
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed
Shein anatarajiwa kuwa mgeni rasmi
katika utoaji wa tuzo za Wanamichezo Bora Tanzania Ijumaa wiki hii.

Tuzo hizo zinaandaliwa na Chama cha
Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania
(TASWA) na mwaka huu zimedhaminiwa na Selcom Wireless, Said Salim Bakhresa & Co Ltd - Bakhresa Group, IPTL, mifuko ya hifadhi ya jamii, PSPF na NSSF.

TASWA inaishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ushirikiano wake na kukubali Rais Dk. Shein aje katika tuzo zetu, ambazo zitafanyika ukumbi wa Diamond Jubilee,
VIP Dar es Salaam.

Kukubali kwa Dk. Shein kuwa mgeni rasmi kunaonesha jinsi gani alivyokuwa
mwanamichezo wa kweli na mwenye nia ya dhati ya kushirikiana na wadau wa
michezo nchini.

Wanamichezo 44 wanatarajiwa kupewa
tuzo siku hiyo baada ya kufanya vizuri
katika michezo mbalimbali kuanzia Juni
2013 hadi Juni 2014. Pia itatolewa Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa jumla na Tuzo ya Heshima.

TASWA imewahi kutoa Tuzo ya Heshima
kwa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu,
Benjamin Mkapa, pia imewahi kutoa Tuzo ya Heshima kwa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ iliyokuwa ikicheza
mechi za kufuzu fainali za mataifa ya
Afrika mwaka 1980 zilizofanyika Lagos,
Nigeria.

Tunaamini zitakuwa tuzo za aina yake,
ambapo tayari Kamati ya Kusimamia Tuzo hizo imeshatangaza majina ya
wanamichezo zaidi ya 100 wanaowania
tuzo mbalimbali.

Ahsanteni
Egbert Mkoko Makamu Mwenyekiti TASWA 10/12/2014

Chapisha Maoni

 
Top