MWANASOKA bora wa dunia, Cristiano Ronaldo atachuana na mshindi wa zamani wa tuzo hiyo, Lionel Messi kwa mara nyingine baada ya orodha fupi ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ya wawania Ballon d'Or kutolewa.
Wawili nyota wa Real Madrid na Barcelona kwa sasa, wote wameingia kwenye orodha ya wachezaji watatu wa mwisho kwa ajili ya tuzo hiyo itakayotolewa mwaka 2015, wakichuana na kipa wa Ujerumani na Bayern Munich, Manuel Neuer.
Ronaldo na Messi peke yao wameshinda tuzo hiyo mara sita baina yao.Mshambuliaji wa kimataifa wa Ureni, Ronaldo mwenye umri wa miaka 29, alishinda tuzo hiyo kwa mara ya pili mwaka jana na anapewa nafasi kubwa ya kushinda tena baada ya kufunga mabao 50 katika mechi 46 za klabu na
timu ya taifa mwaka 2014.
Pia aliisaidia Real kushinda mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la Mfalme na Super Cup ya UEFA.
Mshindi mara nne wa tuzo hiyo, Messi mwenye umri wa miaka 27, ambaye hivi karibuni alivunja rekodi ya jumla ya ufungaji wa mabao katika La Liga, aliiwezesha Argentina kufika Fainali ya Kombe la Dunia na kushinda tuzo ya
Mpira wa Dhababu kama Mchezaji Bora wa Mashindano nchini Brazil.
Neuer, mwenye umri wa miaka 28, alikuwa mmoja wa nyota walioiwezesha Ujerumani kutwaa Kombe la Dunia na pia kushinda Glavu za Dhahabu kama Kipa Bora wa Mashindano.
Pia ndiye kipa namba moja wa klabu na timu yake ya taifa na aliiwezesha pia Bayern kutwaa mataji mawili ya nyumbani msimu uliopita.
Chapisha Maoni