TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Jumatatu, Desemba 8, 2014, ameanza kazi rasmi baada ya afya yake kuimarika kufuatia upasuaji
aliofanyiwa mwezi uliopita.
Mhe. Rais ameanza kazi rasmi kwa kumwapisha Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Daudi Felix Ntibenda katika shughuli fupi
iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam.
Kwa kuanzia Mhe. Rais atakuwa anafanya kazi za ofisini na kwa muda mchache. Muda na kasi ya kufanya kazi ya Mhe. Rais vitaongezeka kwa kadri
afya yake inavyozidi kuimarika.
Na kwa sababu sasa ameanza kazi, Mhe. Rais ataanza kushughulikia mambo yale ambayo yamekuwa yanasubiri maamuzi yake.
Rais Kikwete alifanyiwa upasuaji wa tezi dume katika Hospitali ya Johns Hopkins ya Baltimore, Maryland, Marekani Novemba 8, mwaka huu na alirejea nyumbani Novemba 29, mwaka huu.
Tokea awasili nyumbani, Mhe. Rais amekuwa anafanya mazoezi asubuhi na jioni kuimarisha afya yake kama alivyoshauriwa na madaktari.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
8 Desemba,2014
Chapisha Maoni