0
Wakati Rais Jakaya Kikwete akitarajia kutoa maamuzi juu ya kashfa ya uchotaji wa fedha zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow wiki ijayo, Kampuni ya VIP Engineering and
Marketing Limited, imedai maamuzi ya Bunge yaliyopendekezwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ni ya kipuuzi.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana yenye kurasa 19 na orodha ya vielelezo 17, Katibu wa kampuni hiyo, Respicius Didace, alisema VIP inatuhumiwa kimakosa kwamba
imefanya vitendo vya uvunjifu wa sheria
kuhusiana na Akaunti ya Tegeta Escrow.

“Tuhuma hizi ni upuuzi kwa sababu VIP ililipwa kwa msingi wa Mkataba wa Uuzaji wa Hisa uliotangazwa na kuridhiwa kwa amri ya Mahakama ya Septemba 5, 2013; na kufuatiwa na
amri ya mahakama ya Januari 17, 2014
iliyotolewa katika shauri la wazi; na baada ya kuwa imefanya malipo ya Sh. za Tanzania bilioni 38 (sawa na dola za Marekani milioni 23.6) katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya
kugharimia malipo yote ya kodi ya VIP,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ambayo pia imeishambulia

Benki ya Standard Chartered (SCB) kama
chimbuko la vurugu zote kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow. Didace alisema VIP si mshirika katika mkataba wa akaunti ya Tegeta Escrow na haikuwa na jukumu
lolote lile katika uanzishwaji wake na ulipwaji wa fedha kutoka katika akaunti hiyo na siyo mwanahisa tena wa IPTL.

Didace alisema hoja zilizotolewa na PAC wakati wa mjadala bungeni kwamba fedha zilizopo katika akaunti ya Escrow ni za Serikali siyo sahihi kwani
haikusema wazi ni sehemu gani ya fedha hizo ni mali ya umma na kwa misingi gani.

“ Huo si msingi wenye mashiko wa kuwatuhumu watu kwamba wameiba fedha za umma, VIP ina uelewa mpana na wa kina wa historia ya IPTL na
msingi wake wa kisheria na imegundua kwamba taarifa nyingi na tuhuma kuhusu VIP, IPTL na Akaunti ya Escrow zinafanana kwa kutokuwa
sahihi,” alisema.

Alisema VIP inaamini kwamba umma na Bunge la Tanzania wamedanganywa kwa kuaminishwa tuhuma zisizokuwa za kweli ambazo zitafaidisha malengo ya kigeni na kuwafakarisha Watanzania.

Aliongeza kuwa Bunge na PAC zimedharau masuala ya msingi na kushupalia masuala yasiyokuwa na tija kwa taifa na kwamba mapambano haya yamekuwa na mafanikio na hii
ndiyo sababu SCB imesababisha mkanganyiko kwa kuwalisha Watanzania taarifa za uongo.

Didace alisema PAC imetoa tuhuma nzito za uvunjifu wa taratibu au jinai dhidi ya watu kadhaa bila ya kutoa ushahidi au sababu: “Hiki ni kiwango cha juu cha kutokuwajibika na ambalo
limefanyika kwa maslahi ya muda mfupi ya kisiasa.”
“Ni kiwango cha juu cha kukosa uwajibikaji kwa sababu PAC haiwezi kutoa haki ambazo mahakama ya kisheria lazima itoe kwa watu
binafsi wakati wakitoa maamuzi kuhusu migogoro yao,” imeeleza taaifa hiyo.

Alisema hakuna mahitimisho yoyote ya kisiasa yanayoweza kupewa fursa ya kuathiri mwenendo wa utoaji wa haki na mwenendo mzima wa kisheria wa pande zote za ndani ya Tanzania na nchi za nchi ikiwa ni pamoja na kwa VIP.

“Mihimili ya mahakama na watendaji wa serikali wasikimbilie katika kuhukumu na badala yake waheshimu uhuru, mamlaka ya kisheria na madaraka ya muhimili wa mahakama, ambao ndio
nguzo za utawala wa sheria katika nchi yoyote ile ya kidemokrasia kama Tanzania,”i meeleza taarifa hiyo.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, wabunge walitoa maazimio manane kuhusu sakata la Escrow likiwamo la kutenguliwa kwa nyadhifa za Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Frederick Werema.

Wengine waliopendekezwa kuvuliwa yadhifa zao ni wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge hilo, William Ngeleja (Sheria, Katiba na Utawala), Andrew Chenge (Bajeti) na Victor Mwambalaswa
(Nishati na Madini).

Pia wamo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Viongozi wa umma na maofisa wa ngazi za juu serikalini wanapaswa kuwajibika kwa sababu wamehusishwa na vitendo vya kijinai katika sakata hilo linalohusisha kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania (IPTL).

Kadhalika, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, vimetakiwa kufanya
uchunguzi dhidi ya wote waliotajwa kuhusika na sakata hilo na kupendekeza watakaobainika kuhusika wachukuliwe hatua.

Maazimio mengine ni kumtaka Rais kuunda Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya majaji kuhusishwa
kwenye kashfa hiyo.

Majaji waliotakiwa kuchunguzwa ni Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Prof. Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Aidha, Bunge lilitaka mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Stanbic Bank Tanzania Ltd na benki nyingine yoyote itakayogundulika
baada ya uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika akaunti ya Escrow, kuwa ni taasisi zenye
shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.

Pia, Serikali iandae na kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria iliyounda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahususi
itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi,
kijamii na kisiasa kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo.

Serikali imetakiwa kutekeleza azimio la Bunge kuhusu mikataba mibovu ya kuzalisha umeme kati ya Tanesco na kampuni binafsi ya kufua umeme na hivyo kuwasilisha taarifa ya utekelezaji
wa mapitio ya mikataba ya umeme kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti.

Chapisha Maoni

 
Top