Jeshi la polisi mkoani Kagera linawashikilia watu 12 wanaotuhumiwa kujihusisha katika matukio mbalimbali ya mauaji yakiwemo ya kukatakata
watu kwa mapanga ambao wamekuwa wakikodiwa na wahalifu kwaajili ya kufanya matukio hayo ya
mauaji.
Akiongea na waandishi wa habari Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kagera Henri Mwaibambe amesema katika kipindi cha miezi minne tangu
mwezi wa Agosti mwaka huu mpaka sasa watu sita wameuawa kikatili kwa kukatwa na mapanga.
Kamanda Mwaibambe pia amefafanua kuwa katika uchunguzi wa awali jeshi limebaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni kuwepo kwa imani za
kishirikina.
Kamanda mwaibambe amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kuweza kuwabaini watu wote wanaojihusisha na matukio hayo ambapo amewatoa hofu wananchi wa mkoa huo kuwa jeshi la polisi sasa limeimarisha ulinzi na linaendelea kufanya upelelezi.
Amesema pia kuwa jeshi hilo linaendelea kufanya doria za mara kwa mara katika wilaya zote za mkoa wa Kagera ambako kumekuwa kukitokea
matukio ya namna hiyo na litawatia mbaroni watu wote waliojihusisha na matukio hayo na kuua watu wasio na hatia.
Matukio ya watu kuchinjwa yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika maeneo ya kibeta na kitendaguro ambapo watu sita wameshauawa kwa kuchinjwa akiwemo mwalimu wa shule ya
sekondari kagemu ambae aliuwawa kanisani wakati akifanya maombi.
Chapisha Maoni