MKURUGENZI wa Fedha wa Benki Kuu, Julius Angello, Meneja wa Misamaha ya Kodi wa TRA, Kyabukoba Mutabingwa na Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco, Steven Urassa wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kupokea rushwa ya zaidi ya Sh bilioni mbili
kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Washtakiwa hao walipandishwa jana kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya mahakimu wawili tofauti na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Leonard Swai.
MUTABINGWA
Akisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Janeth Kaluyenda, mshtakiwa Mutabingwa anayekabiliwa na mashtaka manne, alidaiwa kutenda makosa
hayo Januari 27, 2014 maeneo ya Benki ya Mkombozi iliyopo Manispaa ya Ilala.
Inadaiwa mshtakiwa akiwa katika wadhifa wake wa Meneja wa Misamaha ya Kodi wa TRA, alipokea rushwa ya Sh 1, 617,000,000 kupitia akaunti
namba 00110202613801, fedha hizo ni miongoni mwa fedha zilizokuwemo katika Akaunti ya Tegeta Escrow, alipokea kutoka kwa Mshauri wa Kimataifa ambaye ni Mkurugenzi wa VIP Engineering na Mkurugenzi wa zamani wa IPTL, James Rugemalira.
Mshtakiwa anadaiwa kupokea tuzo hiyo kwa kuiwakilisha TRA na wakati huo huo Kampuni ya Mabibo Beer Wines and Spirits inayomilikiwa na Rugemalira katika moja ya kesi zake zilizoko
Mahakamani.
Swai alidai katika shtaka la pili kuwa, Julai 15 mwaka jana maeneo ya Benki ya Mkombozi mshtakiwa alipokea rushwa ya Sh 161,700,000
kupitia akaunti namba 00110202613801, fedha za Escrow kutoka kwa Rugemalira.
“Mheshimiwa shtaka la tatu, inadaiwa Agosti 26 mwaka jana maeneo ya Benki ya Mkombozi, mshtakiwa alipokea rushwa tena ya Sh 161,700,000 kupitia akaunti hiyo hiyo kutoka kwa
Rugemalira na fedha hizo zilikuwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
“Shtaka la nne anadaiwa Novemba 14 mwaka jana kwa kutumia akaunti yake hiyo alipokea rushwa ya Sh 161,700,000 kutoka kwa Rugemalira, fedha
ambazo zilikuwemo katika Akaunti ya Tegeta Escrow,” alidai Swai.
Swai alidai upelelezi wa kesi umekamilika na aliomba tarehe ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.
Pamoja na hilo, Swai alisema mshtakiwa hakuwa na pingamizi la dhamana isipokuwa aliomba Mahakama ifunge akaunti yake mpaka kesi itakapomalizika.
Hakimu Kaluyenda alisema mshtakiwa
atadhaminiwa baada ya kutimiza masharti ya kuwasilisha mahakamani fedha taslimu Sh bilioni moja ama hati ya mali isiyohamishika yenye
thamani hiyo, wadhamini watatu watakaosaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 340 kila mmoja, wadhamini wawili wawe na kazi ya kuaminika, wawasilishe kitambulisho na
mshtakiwa hatakiwi kutoka nje ya Dar es Salaam bila kibali.
Mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti ya dhamana, hati za nyumba hazikuwa na ripoti ya mthamini kuonyesha thamani yake hivyo alirudishwa rumande hadi atakapotimiza masharti,
kesi itasikilizwa Januari 29 mwaka huu na tayari akaunti yake imefungwa.
URASSA
Swai akisoma mashtaka dhidi ya Urassa mbele ya Hakimu Kaluyenda alidai, Februari 14 mwaka jana maeneo ya Benki ya Mkombozi iliyopo wilayani
Ilala, mshtakiwa akiwa Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco alipokea rushwa ya Sh 161,700,000
kupitia akaunti namba 00120102658101 kutoka kwa Rugemalira, fedha zilizokuwemo katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Mshtakiwa anadaiwa kujipatia tuzo hiyo baada ya kuiwakilisha Tanesco na IPTL katika kesi ya Standard Charter nchini Hong Kong.
Urassa alikana mashtaka, upelelezi wa kesi umekamilika, upande wa mashtaka haukuwa na pingamizi la dhamana isipokuwa aliomba akaunti ya mshtakiwa ifungwe kutumika mpaka kesi
itakapomalizika.
Hakimu Kaluyenda alikubali kumpa dhamana mshtakiwa kwa masharti ya kuwasilisha fedha taslimu Sh milioni 81 ama hati ya mali isiyohamishika, wadhamini wawili wafanyakazi,
barua kutoka ofisini na kitambulisho.
Mshtakiwa alitimiza masharti ya dhamana lakini hakuweza kuwasilisha ripoti ya mthamini kujua thamani ya mali yake.
Hakimu Kaluyenda alisema mshtakiwa alishakuwa mfanyakazi wa Tanesco ni wakili hivyo mahakama inakubali kumpa dhamana na upande wa mashtaka waendelee kuhakiki hati. Kesi
itasikilizwa Februari 2 mwaka huu.
ANGELLO
Mshtakiwa Angello alipanda kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Kisoka na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali kutoka Takukuru, Leonard Swai.
Swai alidai mshtakiwa Februari 6 mwaka jana maeneo ya Benki ya Mkombozi, akiwa Mkurugenzi wa Fedha wa BoT alipokea rushwa ya Sh 161,700,000 kupitia akaunti namba 00120102646201 kutoka kwa James Rugemalira.
Fedha hizo zinadaiwa zilikuwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow, alipokea kama tuzo kutokana na malipo yaliyotolewa katika akaunti hiyo kwenda
kwa Pan Africa Solutions Limited (PAP).
Mshtakiwa alikana mashtaka, upelelezi
umekamilika, waliomba tarehe nyingine ya kuanza kusikiliza kesi na waliomba mahakama iamuru kufungwa kwa akaunti ya mshtakiwa.
Hakimu Kisoka alikubali kumpa dhamana mshtakiwa kwa masharti ya kuwasilisha mahakamani fedha taslimu Sh 80,800,000 au hati ya mali yenye thamani hiyo, wadhamini wawili,
kila mmoja asaini dhamana ya maneno ya Sh milioni 50, mdhamini mmoja kutoka serikalini na mwingine anayeishi Dar es Salaam.
Alisema hati ya nyumba lazima iwe na ripoti ya mthamini kuonyesha thamani yake halisi bila hivyo hawezi kutoa dhamana. Mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti, alirudishwa rumande na kesi itaendelea kusikilizwa maelezo ya awali Januari 27 mwaka huu.
Wakati huo huo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, amewasilisha ilani ya kuzuia fedha zilizomo katika akaunti ya Rugonzibwa Mujunangoma anayedaiwa kupokea rushwa ya
zaidi ya Sh milioni 300, aliyefikishwa mahakamani Jumatano ya wiki hii mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru.
Hadi jana washtakiwa watano walikuwa
wamefikishwa mahakamani wakituhumiwa kupokea rushwa kwa Rugemalira kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Chapisha Maoni