0
WATU watano wamekufa baada ya basi aina ya
Super Sami, mali ya Kampuni ya Super Sami
lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda
Mwanza, kugonga jiwe na kupinduka katika
barabara ya Mwanza-Shinyanga eneo la Mabuki
wilayani Misungwi mkoani Mwanza.
Basi hilo lenye namba za usajili T499 BCB,
likiendeshwa na dereva William Elias maarufu
kama Massa (44) ambaye ni mkazi wa Mabibo
jijini Dar es Salaam, lilipata ajali hiyo saa saba
usiku wa kuamkia jana.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed
Msangi alisema baada ya kugonga jiwe dereva
alishindwa kulimudu na kupinduka na
kusababisha vifo vya watu watano akiwemo
dereva, msaidizi wake na majeruhi 13.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva aliyekuwa
kwenye mwendokasi hali iliyosababisha basi hilo
kugonga jiwe lililokuwa barabarani na kushindwa
kumudu basi hilo lililoserereka na kupinduka.
Aliwataja waliokufa kwenye ajali hiyo kuwa ni
Massa ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam, Vaileth
Odede (21) mkazi wa Mwanza, mwanamume
mmoja na wanawake wawili wenye umri kati ya
miaka 25-30 ambao hawajatambulika.
“Majeruhi watano kati ya 13 wamepelekwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Bugando kupatiwa matibabu,
na wengine wanane wanatibiwa katika Hospitali ya
Wilaya ya Misungwi,” alisema Kamanda Msangi.
Aliwataja majeruhi wanaoendelea na matibabu
katika Hospitali ya Misungwi kuwa ni Sophia Miraji
(25), Kibilo Mwacha anayekadiriwa kuwa na miaka
kati ya 35 hadi 40, Boniphace Charles (38-40) na
Frank Munyuni (30).
Majeruhi wengine ni Stanley Zacharia (25), Sia
Dauson (28), Hellen Luheke( 30-35), Michael
Leonard (30-35), Kudra Ibrahim ambaye ni mtoto
wa miaka miwili na miezi 10, Zamda Issa (24),
Marietha Christopher (26), Elizabeth Simon (40) na
Dickson Msamba (22).

Chapisha Maoni

 
Top