0
Baada ya kimya cha muda mrefu, hatimaye
aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Charles Kitwanga ameibuka na kukabidhi ofisi na
akatoa ratiba ya shughuli zake katika Jimbo lake
la Misungwi ikiwamo ibada ya shukrani.
Kitwanga ambaye uteuzi wake ulitenguliwa May
20 na Rais John Magufuli baada ya kuingia
bungeni na kujibu swali akiwa amelewa, alikabidhi
ofisi jana kwa Mwigulu Nchemba ambaye
amechukua nafasi yake.
Baada ya uteuzi wake kutenguliwa, Kitwanga
alitoweka bungeni na baadaye ilielezwa kuwa
alikwenda Israel kabla ya hivi karibuni kurejea
nchini na kusema kuwa yote yaliyotokea
anamwachia Mungu.
Hivi karibuni, Rais Magufuli alimhamishia Mwigulu
katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kutoka
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi huku Dk
Charles Tizeba akimrithi Mwigulu.
Akizungumza katika mahojiano baada ya
kukabidhi ofisi, Kitwanga alisema kila Mtanzania
anaweza kufanya kazi iwapo atapewa nafasi huku
akinukuu kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ na kwamba
amefanya makabidhiano hayo kwa wema na
upendo wa hali ya juu.
Alisema amekabidhi ofisi bila kinyongo kwa
sababu Tanzania si nchi yake peke yake bali ni ya
wananchi wote.
Ratiba jimboni
Akizungumzia ratiba jimboni mwake, Kitwanga
alisema Agosti 6, atafanya ibada ya shukrani
nyumbani kwake Misungwi kumshukuru Mungu
akisema hiyo ni baada ya ziara yake ya wiki sita
mfululizo kwa wapigakura wake.
Ziara hiyo itaanza keshokutwa atakapokutana na
kamati ya mipango na fedha kabla ya kufanya
kikao na madiwani wote wa jimbo hilo Jumamosi
ijayo.
Alisema Jumatatu ijayo atakabidhi vifaa
mbalimbali vikiwamo magodoro na vitanda kwa
hospitali ya wilaya na zahanati, vyerahani na
kompresa kwa vikundi za ujasiriamali katika hafla
itakayofanyika kwenye Stendi ya Mabasi
Misungwi: “Hapo nitatoa nafasi ya dakika 10
mpaka 20 kwa waandishi wa habari kuniuliza
maswali... lakini nisingependa umbeya... kwangu
mimi ni Tanzania kwanza, nawaambia kabisa.”
Baada ya shughuli hiyo, alisema siku inayofuata
atakutana na wenyeviti wa vijiji vyote vya jimbo
hilo kupanga namna atakavyofanikisha ziara yake
katika maeneo yao, kazi ambayo alisema
ataifanya kwa wiki sita mfululizo; “nitafanya ziara
siku tano kwa kila wiki mfululizo, zamani nilikuwa
nikigawa muda wa kutembelea jimbo na kurudi
Dar kufanya kazi sasa nitakuwa huko muda wote.
Dar nitakuwa nakuja mara chache tu.”

Chapisha Maoni

 
Top