Raphael Makongojo (25) aliyembaka aliyekuwa
mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya
Wasichana ya Korogwe amehukumiwa kifungo
cha miaka 30 jela.
Pia Makongojo amepewa adhabu kali, ikiwemo
viboko 12 pamoja na kuamriwa kutoa faini ya
Sh milioni 15 mara atakapomaliza kifungo
chake.
Hukumu hiyo iliyotolewa na Mahakama ya
Wilaya ya Arusha ndani ya chumba cha
faragha (chemba) ambako waandishi
hawakuruhusiwa kusikiliza hukumu, lakini
baadaye waliambiwa kwa sharti la hakimu
wala waendesha mashtaka kutajwa majina yao
kwa sababu kesi hiyo iliendeshwa faragha.
Awali kesi hiyo ilianza kwa mshitakiwa
kusomewa maelezo yake ya awali akituhumiwa
kumbaka mwanafunzi wa Kidato cha Sita wa
Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Korogwe
ambaye hivi sasa amemaliza masomo.
Awali askari huyo alishushwa pamoja na
mahabusu wenzake mahakamani hapo, lakini
kwa kuwa kesi inayomkabili ni ya ubakaji
hivyo inasikilizwa ndani ya chumba cha
faragha (chemba) ambako hakuna ruhusa kwa
wanahabari kuandika habari hiyo hadi hapo
hukumu itakapotolewa.
Kwa mujibu wa Kifungu cha Sheria Namba
186 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa
ya Jinai Sura ya 20 ya Mwenendo wa Makosa
ya Kujamiiana ya Mwaka (1998) inayosema
kuwa bila kujali masharti ya sheria nyingine
yoyote inayohusisha makosa ya kujamiiana,
ushahidi au mashahidi watakaohusika
hawaruhusiwi kutolewa kwenye chombo
chochote cha habari.
Awali, mshitakiwa huyo kwa mara ya kwanza
alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa
shtaka lake kwa hakimu (jina linahifadhiwa)
ambako Wakili wa Serikali (jina linahifadhiwa)
alidai mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa
huyo alitenda kosa hilo Januari 16, mwaka
huu katika eneo la Kwa Mrombo, FFU jijini
Arusha.
Alidai kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa
hilo kinyume cha Kifungu cha 130(1 na 2 a)
cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai,
Sura ya 16.
Baada ya hukumu hiyo kutolewa, mama mzazi
wa mtoto huyo ambaye hakupenda kutaja jina
lake, aliiomba serikali kuingilia kwa makini
sheria inayohusu makosa ya ubakaji ili adhabu
itakayotolewa kwa mbakaji iwe kifungo cha
maisha badala ya hakimu au mahakama kutoa
kifungo cha miaka 30.
Chapisha Maoni