Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 2
ya mwaka 2016 ambayo pamoja na mambo
mengine, imeongeza adhabu kwa watu
wanaowapa mimba au kuoa ama kuolewa na
mwanafunzi, sasa watafungwa jela miaka 30.
Sheria hiyo ilipitishwa jana bungeni mjini
Dodoma baada ya Muswada kuwasilishwa Juni
24, mwaka huu na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG) ambao baadhi ya wabunge
walipata fursa ya kuuchangia.
Muswada huo ulilenga kufanya marekebisho
katika sheria 21 kwa lengo la kuondoa
mapungufu yaliyobainika wakati wa utekelezaji
wa sheria hizo na umepitishwa kuwa sheria.
Sheria zilizopendekezwa kurekebishwa na
sheria hiyo ni pamoja na ya Kudhibiti
Utakatishaji wa Fedha Haramu; Kudhibiti
Usafirishaji Haramu wa Binadamu; Kanuni za
Madai; Usajili wa Makandarasi; Elimu; Ajira na
Mahusiano Kazini na Sheria ya Taasisi za
Kazi.
Muswada huo uliowasilishwa bungeni na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju
unatamka adhabu ya kifungo cha miaka 30
jela katika marekebisho ya Sheria ya Elimu
kwa watakaompa mimba, kumuoa au kuolewa
mwanafunzi.
Awali adhabu iliyotamkwa katika sheria hiyo
ya elimu ni mshitakiwa akibainika kuwa na
kosa kutozwa faini ya Sh 500,000 na iwapo ni
kosa la pili anatozwa faini ya Sh 500,000 au
kifungo kisichozidi miaka mitatu.
Akiizungumzia sheria hiyo inayosubiriwa
kusainiwa na Rais John Magufuli, Masaju
alisema inawalinda watoto wote chini ya miaka
18 walioko na wasio shuleni na kuwa kosa
hilo likifanywa na mtoto atahukumiwa kwa
mujibu wa sheria ya mtoto.
Kifungu cha 60 A (i) kimeeleza kuwa itakuwa
kinyume cha sheria katika mazingira yoyote
yale kwa mtu yeyote kumuoa au kuolewa na
mwanafunzi wa shule ya sekondari au ya
msingi na atakayekiuka atafungwa jela miaka
30.
Katika Sheria ya Taasisi za Kazi inataka
mwajiri anapokiuka masharti ya sheria ya kazi,
ikiwa ni pamoja na kuchelewesha michango ya
waajiriwa, kutoza faini na Ofisa wa Kazi ya
papo kwa hapo isiyopungua Sh 100,000.
Wakichangia muswada huo, wabunge
wameonesha furaha yao juu ya Sheria ya
Elimu inayohusu adhabu ya miaka 30 jela.
Hata hivyo, pamoja na furaha hiyo, baadhi ya
wabunge wametoa angalizo la kutaka kupimwa
kwanza DNA kabla ya kutoa hukumu huku
wengine wakitaka kuwapo kwa nyongeza ya
viboko.
Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu
(CCM) alipongeza marekebisho hayo na kutaka
adhabu ya miaka 30 iongezwe na kuchapwa
viboko 12 kila mwezi mpaka aliyehukumiwa
anamaliza kifungo kutokana na wahalifu hao
kuwa na mazoea ya kuzoea gereza.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Subira Mgalu
(CCM) alisema pamoja na serikali kuja na
marekebisho hayo pia waangalie namna ya
kukabiliana na utoro shuleni ili kuwafanya
wanafunzi kupata elimu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Njombe Kusini,
Edward Mwalongo (CCM) alitaka sheria imtake
anayekutwa na kosa hilo kuacha fedha za fidia
ambazo mama atazitumia wakati mwanaume
akiwa jela.
Akijibu hoja ya kutumika kwa vipimo vya
vinasaba (DNA), Masaju alisema kwa sasa
utaratibu wa vipimo hivyo utatumika
mahakamani na waendesha mashitaka
kuhakikisha hawaachi shaka kwenye ushahidi
kutokana na Tanzania kutokuwa na uwezo wa
kumpima DNA mtoto akiwa tumboni.
Kuhusu Sheria ya Taasisi za Kazi, Mbunge wa
Viti Maalumu, Hawa Chakoma (CCM), alitaka
adhabu hiyo kuongezwa ili sheria kuleta tija
na kutaka kazi ya kutoza faini hiyo isifanywe
na Ofisa wa Kazi kama ilivyotamkwa katika
sheria badala yake ifanywe na Mamlaka ya
Usimamizi wa Mifuko ya Jamii (SSRA)
kutokana na mifumo mizuri ya ufuatiliaji.
Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama
alisema serikali imekuja na sheria hiyo ili
kuwabana waajiri wanaochelewesha michango
ya waajiriwa na kuwa katika kutekeleza sheria
waziri ataweka makundi na kuwa kampuni
zenye kipato kikubwa adhabu yao itakuwa
kubwa zaidi.
Chapisha Maoni