Wabunge wa chama hicho kuwapa barua za
kujieleza wabunge wao wasiohudhuria,
wanaochelewa na wanaondoka kabla ya vikao
vya Bunge kuahirishwa.
Tayari maagizo hayo yamefanyiwa kazi na
Katibu wa Wabunge wa CCM, Jasson Rweikiza
ambaye amewalima barua wabunge hao.
Katika barua yenye kichwa cha habari
“Maagizo ya Kamati Kuu ya CCM” aliyopewa
mmoja wa wabunge wa CCM inaonyesha
wametakiwa kujieleza kwa nini siku nyingine
walifika wamechelewa na mara kadhaa
walitoka mapema kabla kuahirishwa kwa
Bunge.
“Mwenendo huu ni kukiuka kanuni za Kamati
ya Wabunge wote wa CCM hasa kanuni ya 41.
Tafadhali andika maelezo kwa nini Kamati Kuu
isichukue hatua? Maelezo yanifikie kabla ya
Juni 25 mwaka huu,” ilisema sehemu ya
barua ya mmoja wa wabunge walioandikiwa.
Alipoulizwa Rweikiza kuhusiana na barua hiyo
alisema haitambui na kwamba imeghushiwa.
“Kanuni zipo zinazoongoza vikao vya Bunge,
zipo pia zinazoongoza wabunge wa CCM.
"Wakitaka kuondoa wabunge wa CCM
wanazijua sana, isipokuwa hatujafikia hatua ya
kufundishana kwa kuanza kuandikiana
barua,”alisema.
“Wanajua mbunge hawezi kuondoka bila
kwenda kwa Spika na kuomba ruhusa au
kujulisha kwenye chama kwamba anatoka,
wanajua,” alisema Rweikiza na kusisitiza
kwamba hata taarifa zinazoonyesha kuna
wabunge wanaotakiwa kujieleza kwake ni
majungu tu.
Japokuwa Rweikiza ameikana barua hiyo,
wabunge kadhaa wa CCM walioomba majina
yao yasitajwe wamekiri kwamba barua hizo
zimetolewa na kwamba wanabanwa kwa
kutakiwa kujisajili mara mbili; kitabu cha
Bunge na cha CCM.
Katika ukurasa wake wa Facebook
uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii,
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter
Msigwa (Chadema), alisema wabunge wa CCM
wanalalamikia kulazimishwa kuingia bungeni
kwa kuwa Bunge halina ladha.
Pia, Msigwa alisema wabunge hao wa CCM
wanadai Naibu Spika Dk Tulia Ackson hafuati
kanuni na taratibu na kwamba wametakiwa
kujieleza Kamati Kuu ya CCM.
Aidha, baadhi ya wabunge wa CCM
walionekana kukerwa na utaratibu wa kujisajili
sehemu mbili yaani Bunge na CCM mara mbili
kwa siku.
“Kuna haja gani ya kutia dole (kusaini kwa
utaratibu wa kieletroniki) halafu tena tuje
tusaini kwenye makaratasi ya CCM?,” alihoji
mmoja wa wabunge.
Alisema ili kusaini karatasi hizo inawapasa
wabunge kwenda upande wa Kambi Rasmi ya
Upinzani ambapo wabunge waliokabidhiwa
kazi ya kuzitunza karatasi hizo hukaa kama
kambi mbadala baada ya wabunge wa
upinzani kususia vikao vinavyoendeshwa na
Dk Tulia.
“Wengine tunaheshima zetu hatuwezi kwenda
upande wa upinzani kufuata makaratasi ya
kusaini. Kwanza Bunge lenyewe halina mvuto
unakuja hapa watu wawili ndio wanapewa
nafasi ya kuchangia mjadala na baada ya hapo
wanapitisha,” alisema.
Mbunge mwingine wa CCM alisema haoni haja
ya kuwepo ndani ya Bunge kwa sababu
hawapewi nafasi ya kutosha ya majadiliano na
hivyo bora kutokuwepo ndani ya ukumbi muda
wote.
“Mimi saa hizi naingia ndani ya ukumbi wa
Bunge nasaini natoka naenda zangu kantini
(ya Bunge) kuangalia mpira maana hata
nikikaa ndani sitopata nafasi ya kuchangia,”
alisema mbunge huyo.
Alisema haoni haja ya kusaini mara mbili kwa
sababu CCM wanaweza kutumia usajili wa
Bunge kufahamu wabunge waliopo na
wasiohudhuria kwa wakati wanaouhitaji.
Alisema orodha hiyo haina mashiko kwa
sababu wanazo namba za wabunge wote
kama kuna jambo ambalo wanahitaji basi
wanaweza kuwataarifu.
“Hata mimi nimepewa barua ya kujieleza lakini
si kwamba ni mtoro bali tunakuwa na
majukumu mengine ya kibunge nje ya Bunge,”
alisema.
Hatua hiyo inakuja wakati wabunge 118 wa
vyama vinavyounda Ukawa, wakiwa
wamesusia vikao vya Bunge vinavyoendeshwa
na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kwa madai
ya kuongoza vikao kibabe na kutofuata
kanuni.
Hii ni wiki ya nne tangu Dk Tulia aanze
kuendesha vikao vya Bunge peke yake bila
kupokewa na wenyekiti wa Bunge kama
ilivyokuwa kabla hajatofautiana na kambi
rasmi ya upinzani
Chapisha Maoni