0
MAREKEBISHO ya Sheria mpya ya Manunuzi,
yamewasilishwa bungeni yakitamka kufyeka
posho za watendaji, wanaosimamia mchakato wa
zabuni na kuondoa vikao vya bodi kutoka 12 kwa
mwaka hadi vinne, ikisisitiza kuziba mianya ya
rushwa na kuongeza uwazi.
Aidha, muswada wa marekebisho hayo, unataka
kampuni au mshauri wa nje ili apewe zabuni
katika shughuli zinazogharimiwa na fedha za
umma, ahakikishe asilimia 60 ya wafanyakazi wa
kampuni yake ni Watanzania.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango,
aliyasema hayo jana mjini Dodoma wakati
akiwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria
ya Ununuzi wa Umma wa Mwaka 2016.
Kupungua kwa vikao vya bodi, kumeelezwa na Dk
Mpango kuwa kutapunguza gharama
zinazotokana na posho ya vikao vya bodi ya
zabuni na ada zinazolipwa kwa kamati
zinazohusika na mchakato ya zabuni.
Aidha, posho zinazotokana na utekelezaji wa
majukumu ya kazi ya kila siku ya washiriki
itafutwa. Hata hivyo, imeruhusu kuwapo kwa
vikao vya dharura pale Mwenyekiti wa Bodi akiona
ni lazima.
Pamoja na kupunguzwa vikao, muda wa zabuni
nao umepunguzwa na pia taasisi nunuzi
itaruhusiwa kufanya majadiliano ya bei wakati wa
mchakato wa zabuni kwa lengo la kupunguza bei
ya ununuzi na kuongeza bei ya kuuza mali za
serikali.
Dk Mpango alisema sheria hiyo mpya, itaziba
mianya ya rushwa, kuongeza kasi, uwazi,
uwajibikaji na kuleta upendeleo maalumu kwa
kampuni za Tanzania katika zabuni za ndani na
za kimataifa.
Pia sheria hiyo itaongeza ufanisi na kupata
thamani halisi ya fedha, inayotumika kwa
kununua huduma na bidhaa.
Dk Mpango alisema pamoja na kuongeza
uwajibikaji, sheria hiyo mpya itapunguza vikao
vya bodi hadi kuwa kimoja kwa robo mwaka na
vikao vya dharura, kufanyika pale ambapo
mwenyekiti ataona inabidi.
Pamoja na maelekezo hayo mapya, serikali pia
itaanza kununua bidhaa na huduma kwa bei
inayoendana na bei ya soko, iwapo wabunge
watapitisha marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa
Umma.
Pamoja na ununuzi wa bei ya soko, sheria mpya
imelenga kuweka sharti la kisheria kutoa
upendeleo katika zabuni mbalimbali, hasa kwa
makundi maalumu kama vile wanawake, vijana,
wazee na watu wenye mahitaji maalumu.
Alieleza kuwa sheria mpya imelenga kuiwezesha
serikali, kunufaika na matumizi ya viwango na
kuweka sharti la kisheria la kutumia mifumo ya
kuongeza uwazi katika ununuzi ili kuongeza
uadilifu na uwajibikaji.
Kwa mujibu wa waziri, sheria mpya imelenga
kurahisisha ununuzi wa umma na kuipa faida
serikali baada ya kuwapo kwa changamoto nyingi
kwa Sheria Namba 7 ya Mwaka 2011, ambayo
ilianza kutekelezwa mwaka huo.
Changamoto hizo ni pamoja na bei ya juu ya
bidhaa na huduma zinazonunuliwa na serikali
kulinganisha na bei ya soko kutokana na zuio la
majadiliano kuhusu bei kati ya taasisi nunuzi na
mzabuni.
Pamoja na changamoto ya bei, kumekuwepo na
muda mrefu wa mchakato, gharama kubwa
zinazotokana na matangazo na vikao mbalimbali
vya kupitia zabuni, kutozingatiwa kwa viwango na
kutokuwepo kwa upendeleo katika ushiriki wa
zabuni kwa makundi maalumu.
Mapendekezo ya muswada huo, pia yametaka
pale kampuni au taasisi ya umma inapolazimika
kufanya ununuzi kutoka nje ya nchi, hasa kama ni
suala la ushauri linafanywa na kampuni ya nje ya
nchi, ofisi hiyo ya serikali inalazimika kuhakikisha
kuna wataalamu wa ndani ya nchi.
Aidha, kampuni au mshauri huyo wa nje ili apewe
zabuni katika shughuli ambazo zinagharimiwa na
fedha za umma, kuna kigezo cha kuhakikisha
wafanyakazi wa kampuni yake, zaidi ya asilimia
60 ni Watanzania.
Mbali na kuwa na asilimia 60 ya wafanyakazi
Watanzania, kampuni husika lazima ieleze
kiwango cha bidhaa na huduma zinazozalishwa
ndani ya nchi, ambazo itazinunua katika
utekelezaji wa shughuli zake.
Nayo Kamati ya Bunge ya Bajeti imeitaka serikali
kusimamia na kuhakikisha kwamba watumishi wa
umma ambao hawastahili kupewa magari,
watumie magari yao binafsi ; na wale ambao
wanastahili wakopeshwe magari na serikali na
kupewa posho kidogo kwa ajili ya mafuta na
matengenezo.
Pia, imeitaka serikali iandae utaratibu wa kununua
magari kwa pamoja yasiyo na gharama kubwa
kulingana na bei ya soko.
Akisoma maoni ya Kamati ya Bunge ya Bajeti
kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya
Ununuzi wa Umma wa mwaka 2016, Mwenyekiti
wa Kamati hiyo, Hawa Ghasia alisema kamati
imekubaliana na serikali kufanya manunuzi kwa
kuzingatia thamani ya fedha kwa bidhaa, ikiwamo
manunuzi ya magari
Alisema muswada huo unaonesha kwamba
inawezekana kupunguza gharama za serikali kwa
kufuata thamani ya fedha.
Aidha kamati hiyo imeishauri serikali kuanzisha
mfuko wa uwezeshaji wa makandarasi ili waweze
kumudu utoaji wa huduma mbalimbali,
zinazohuisha gharama kubwa, mfano ukandarasi
wa barabara.
Mfuko huo utakuwa ukitoa dhamana. Pia kamati
hiyo inataka kujua mwanzo wa matumizi ya
sheria mpya.
Wabunge waliochangia muswada huo, waliitaka
serikali nayo kujiunga katika sheria hiyo kwa
kuona kwamba inawalipa wazabuni mapema au
inaeleza watakavyoweza kuwa wazabuni
wanapochelewesha malipo, hasa kutokana na
kampeni yake ya ununuzi kwa bei ya soko.
Wabunge hao walisema kwamba serikali inajua
sababu za bei kubwa na hivyo inafaa ikajipanga
kuondoa kasoro hiyo ili hiyo sheria iweze
kutekelezeka.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Ligora (CCM) alitoa
tahadhari kwamba sheria inabadilishwa Ibara 40
ambayo ni sehemu kubwa na kusema kwamba
lazima ijiandae kuondoa sababu za bei kubwa na
pia kutofuta kipengele cha kamati ya mipango na
fedha kwenye halmashauri kupitia zabuni kwa
lengo la kujiridhisha.
Kauli ya kutofuta kipengele hicho katika muswada,
pia ilizungumzwa na wabunge waliochangia jana.
Aidha wengine walitaka kuwapo na dirisha kwa
ajili ya dharura na hasa dirisha kwa ajili ya bidhaa
za afya na tiba. Wabunge wengine waliochangia ni
Martha Mlata, Rita Kabati, Ali Hassan, Dk
Diodorus Kamara, Japhet Asunga, Adadi Rajab,
Jitu Son, John Kadutu na Amina Mollel.

Chapisha Maoni

 
Top