0
Siku chache baada ya Uingereza kuamua kujitoa
katika Umoja wa Ulaya (EU), Balozi wa nchi hiyo
nchini amesema wataendelea kuimarisha
uhusiano na Tanzania ili kuhakikisha uwekezaji
haupungui.
Akijibu swali kuhusu athari zozote
zitakazojitokeza kwa Tanzania baada ya
Uingereza kujitoa EU, Balozi wa Uingereza nchini,
Dianna Melrose alisema jana kuwa haitapunguza
uwekezaji, misaada wala vita dhidi ya rushwa na
uhalifu wa kimtandao.
“Uhusiano wetu utaendelea kuwa imara kama
ulivyokuwa awali,” alisema Melrose.
Balozi Melrose alisisitiza kuwa Uingereza
itaendelea kuwa mwanachama katika Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa
Kujihami wa Nchi za Magharibi (Nato), Umoja wa
nchi saba zilizoendelea zaidi duniani (G7), umoja
wa mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu
kutoka nchi zenye uchumi mkubwa duniani (G20)
na Jumuiya ya Madola na kushirikiana na
Tanzania.
Tangu Juni 23 Uingereza ilipopiga kura ya maoni
kujitoa EU, umetokea mtikisiko mkubwa kati ya
England na washirika wake Wales, Scotland na
Ireland Kaskazini.
Kura hiyo ya maoni imesababisha Waziri Mkuu,
David Cameron kutangaza kujiuzulu kwa
kushindwa kwake kushawishi nchi hiyo kubaki
EU.
Mtikisiko mwingine mkubwa umejitokeza katika
masoko ya hisa ambapo tangu Alhamisi iliyopita
yameporomoka na kupoteza Dola za Marekani
trilioni mbili.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es
Salaam (DSE), Moremi Marwa alisema soko lake
na mengine Uingereza ni miongoni mwa nchi nne
zenye mchango mkubwa wa kifedha kwa EU.
Takwimu zinaonyesha kuwa kwa mwaka jana
pekee ilichangia Pauni 12.9 bilioni (zaidi Sh37.5
trilioni).
Kiasi hicho ni kikubwa kwa Sh10 trilioni ya bajeti
ya Tanzania kwa mwaka ujao wa fedha,
2016/2017.
“DSE haijaunganishwa sana na masoko ya nje
lakini tunao wawekezaji wengi kutoka Uingereza,”
alisema Moremi na kubainisha kuwa, mabadiliko
yanaweza yakaonekana Soko la Hisa la
Johanessburg (JSE), Afrika Kusini.
Alipoulizwa Katibu Mkuu wa Viwanda na
Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda kwamba Serikali
imejipanga vipi kukabiliana na athari
zitakazojitokeza baada ya Uingereza kujitoa
alisema ni mapema sana kwa wizara yake na
Tanzania kwa ujumla kutetereka kwa namna
yoyote kwa sasa kwa kuwa uhusiano mkubwa
uliopo ni ule wa kiuwekezaji.
“Uwekezaji siyo suala la siku moja,” alisema na
kufafanua kuwa mikataba ambayo ilishatiwa saini
ni lazima itekelezwe kama makubaliano
yalivyofanywa. “Masoko ya hisa ndiyo
yanayoweza kuathirika kwa muda huu mfupi,”
aliongeza.
Mkurugenzi wa Uhusiano na Sheria wa Shirikisho
la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Hussein
Kamote alisema muda huo wa utekelezaji wa
maadhimio ya kujitoa ni mrefu na huenda hatua
za haraka zikachukuliwa kabla athari za kiuchumi
hazijasambaa duniani kote.

Chapisha Maoni

 
Top