0
ALIYEKUWA Mbunge wa Biharamulo Magharibi
kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Dk. Anthony Mbassa
alifariki dunia jana usiku akiwa usingizini
nyumbani kwake.
Taarifa zilizopatikana kutoka Biharamulo na
kuthibitishwa na Msemaji wa familia, Pendo
Ngonyani, zilieleza kuwa kifo cha Dk. Mbassa
kilifahamika alfajiri ya jana.
Alisema watoto walipokwenda kumuamsha
hakuamka hali iliyowalazimu kumuita mama
yao ambaye aliwasiliana na madaktari wa
Hospitali ya Biharamulo na kuthibitishwa kuwa
alikuwa amefariki dunia.
Dk. Mbasa ambaye alikuwa mbunge mwaka
2010 baada ya kushinda uchaguzi mkuu,
hakurejea kwenye ubunge baada ya kuangushwa
na mshindani wake, Oscar Mkasa wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mkuu wa
Oktoba, 2015.
Akizungumzia kifo hicho, Pendo ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema
(Bawacha) Mkoa wa Kagera, alisema Dk. Mbassa
alifariki dunia akiwa usingizini.
Pendo alisema haijafahamika sababu ya kifo
chake ingawa familia imedokeza inataka
uchunguzi ufanyike kubaini sababu ya kifo
hicho.
Kwa mujibu wa maelezo ya familia, juzi mkewe
akiwa kazini, yeye (Dk. Mbasa) alitoka na kurudi
jioni saa 12 na kuacha gari lake nyumbani na
kwenda ambako hakujajulikana. Alirudi
nyumbani saa 5.00 usiku akiwa akionekana
kuwa amelewa.
“Nimeelezwa kuwa baada ya kuacha gari alitoka
kwa mguu kuanzia hiyo saa 12 na kurejea
yumbani saa 5.00 usiku. Haijajulikana
alikwenda wapi lakini alirejea akiwa amekunywa
alikuwa akihangaika na ilidhaniwa ni hali ya
pombe, ndiyo hivyo asubuhi alikutwa akiwa
amefariki dunia.
“Leo alikuwa na safari ya kwenda Bukoba
kuwasiliana na mawakili wake kwa ajili ya
kushughulikia madai ya fidia ya Sh milioni 60 za
gharama za kesi namba 5/2010, iliyofunguliwa na
aliyekuwa mgombea ubunge wa CCM jimbo hilo,
Oscar Mkasa,” alisema.
Alisema kinachosubiriwa hivi sasa ni ndugu na
jamaa kupanga utaratibu wa maziko.

Chapisha Maoni

 
Top