0
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amekemea
matukio ya mauji yanayoendelea nchini na
kusema kuwa hakuna dini inayofundisha vitendo
hivyo viovu.
Alisema serikali inawaomba viongozi wa dini
nchini kuendelea kushirikiana nayo kutoa elimu
kwa waumini wao kama njia ya kukomesha
mauaji dhidi ya watu wasiokuwa na hatia nchini.
Akizungumza Dar es Salaam jana katika fainali ya
mashindano ya kimataifa ya kuhifadhi Koran
nchini, alisema ni wajibu kwa Watanzania
kushikana kulinda amani ya nchi.
“Napenda nigusie mambo machache ambayo
nimeyaona; ni hivi karibuni nchi yetu ilingia
katika mtihani ambao wengi wenu kupitia vyombo
vya habari mliarifiwa juu ya kuuawa kwa waumini
wema waliokuwa wakifanya ibada ndani ya msikiti
kule mkoani Mwanza.
“Katika siku za hivi karibu kumekuwa na matukio
mabaya mbele ya macho yetu na nchi yetu
imefika mahala hadi watu wanafuatwa majumbani
na kuchinjwa jambo ambalo kwetu sisi kama
Serikali tuna kazi ya kulinda uhai wa kila
Mtanzania.
“Linapotokea suala kama hili hatuwezi kula wala
kulala mpaka tuone juhudi za dhati katika
kukomesha unyama wa aina hii,” alisema
Majaliwa.
Alisema Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na
usalama inaendelea kushughulikia tatizo hilo kwa
umakini na akawataka Watanzania kuendelea
kutoa ushirikiano.
Akizungumzia utendaji wa Serikali ya awamu ya
tano, alisema watendaji wengi ni wapya huku
akiomba kukoselewa inapokosea jambo ambalo
litasaidia kujenga Serikali imara na yenye
mshikamano.
Mashindano hayo ya kuhifadhi Koran yalihusisha
washiriki 21 kutoka mataifa mbalimbali duniani
huku kijana, Rashid Ally (8) kutoka Tajikistan
akiibuka mshindi wa kwanza.

Chapisha Maoni

 
Top