0
Hukumu ya kesi ya mauaji ya mwandishi wa
habari wa kituo cha televisheni cha Channel 10,
Daudi Mwangosi itatolewa Julai 21 baada ya
Mahakama Kuu kusikiliza majumuisho na maoni
ya Baraza la Wazee. Kesi hiyo inamkabili askari
wa kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani
Iringa, Prisifius Simon.
Akitoa majumuisho ya kesi hiyo jana, Jaji Paul
Kihwelo alisema ni wajibu wake kutoa
majumuisho kwa kuangalia mazingira na ushahidi
uliomgusa moja kwa moja mtuhumiwa.
Jaji Kihwelo alieleza mahakama kuwa askari huyo
anatuhumiwa kufanya mauaji hayo kwa kukusudia
Septemba 2, 2012.
Alieleza kuwa jukumu la kuthibitisha kosa kwa
mtuhumiwa ni upande wa mashtaka na
wanatakiwa wathibitishe bila kuacha wasiwasi
wowote na si jukumu la upande wa pili
kuthibitisha kuwa mtuhumiwa hakutenda kosa.
Alitaja vielelezo ambavyo vilitolewa mahakamani
bila kupingwa kuwa ni pamoja na ramani ya tukio,
taarifa ya uchunguzi ya kifo cha marehemu,
ungamo la mtuhumiwa na kitabu cha kuchukilia
silaha ofisi za FFU.
Akisoma majumuhisho kwenye upande wa
ungamo, Jaji Kihwelo alisema maungamo
yanayofanywa mbele ya mlinzi wa amani,
yanaweza kutumika kutoa ushahidi.
Mtuhumiwa huyo alieleza mahakama wakati
akitoa ushahidi wake kuwa kabla ya kufika kwa
mlinzi wa amani, aliitwa kuhojiwa na RPC na RCO
ndipo akaenda kufanya ungamo na kwamba
hakufanya chochote zaidi ya kuambiwa asaini.
Akitoa maoni yake mmoja wa wazee wa
mahakama, Khadija Husein alisema baada ya
kusikiliza mashahidi wa pande zote kuanzia
mwanzo hadi mwisho, wamegundua kuwa
mtuhumiwa alienda kufanya ungamo kwa mlinzi
wa amani akiwa huru na kusaini.
Khadija alisema si rahisi mtu kusaini kitu
ambacho hajakitolea maelezo, hivyo alichokisaini
ndicho alichokitenda na alitoa ungamo akiwa huru
bila kupigwa wala kutishiwa
Alisema endapo maelezo hayo yalikuwa si yake,
yangepingwa mbele ya mahakama na wakili wake
au yeye mwenyewe, lakini kwa kuwa yalipokelewa
bila kupingwa hivyo ana hatia ya kutenda kosa
bila kukusudia.
Mzee mwingine, Said Mbaga alipingana na
maelezo hayo, akisema mtuhumiwa hana hatia
kwa sababu shahidi wa kwanza hakuthibitisha
kuwa alitenda kosa kwa sababu hakumuamuru
kupiga bomu.
Mzee wa tatu, Sophia Ng’anguli alisema
mtuhumiwa alitenda kosa bila kukusudia licha ya
ushahidi wa upande wa mashtaka kuacha
mashaka.
Alidai kitu cha msingi kinachomfunga mshitakiwa
ni ungamo alilolitoa kwa mlinzi wa amani, ambalo
aliandika na kusaini huku akikiri na kujutia
kusababisha kifo cha Mwangosi.

Chapisha Maoni

 
Top