0
SIKU chache baada ya kufikishwa katika kituo
maaulum cha kusaidia waathirika wa dawa za
kulevya Bagamoyo Sober House, meneja wa
kituo hicho, Godwin Msilo ameeleza mazito ya
mrembo huyo sambamba na maendeleo yake
kwa ujumla.
Ray C
Ray C alifikishwa kwenye kituo hicho Ijumaa
iliyopita baada ya kukamatwa na polisi maeneo
ya Kinondoni jijini Dar akifanya vurugu baada ya
kudaiwa kuzidiwa na ulevi wa madawa ya
kulevya.
Akizungumza na wanahabari wetu Jumanne
iliyopita katika kituo hicho, meneja huyo alisema
kilichomponza Ray C hadi arudie kwenye
matumizi ya madawa ya kulevya kwa mara ya
pili baada ya awali kupatiwa tiba katika Hospitali
ya Mwananyamala jijini Dar, ni aina ya tiba hiyo
kwani ilikuwa ikimpa mwanya wa kurudia kwenye
matumizi ya madawa hayo.
Alisema, wao wanaamini tiba sahihi ya mtu
aliyetopea kwenye madawa ya kulevya ni
muathirika kufikishwa Sober House kwani wao
wanamfanya muathirika asiweze kukutana na
watu wengine wanaoweza kumshawishi arudie
madawa hayo hatari.
Kwa mujibu wa meneja huyo, kitendo cha kumpa
dawa pekee (methadone) za kumtibu muathirika
wa madawa ya kulevya kisha kumuacha arejee
mtaani ni tatizo kubwa lililofanyika awali kwani
kilimpa mwanya mrembo huyo kujichanganya na
watumiaji wa madawa ya kulevya mitaani.
“Huwezi kumtibu mtu kwa kumpa dawa halafu
ukamwacha muathirika arudi nyumbani, utakuwa
umemjenga vipi kisaikolojia? Kuna haja ya
kumchukua muathirika kumuweka sehemu katika
kituo kama hiki, anapata dawa, akishapata dawa,
anapata elimu anakutana na madaktari wa afya ya
akili, anakutana na madaktari wa saikolojia,
wanamjenga kisaikolojia.
“Huwezi kumwacha tu, arudi nyumbani. Hujui
anakula vipi, anaishije, hiyo haipo. Hivi vitu
vinataka mtu ajitoe kwelikweli, apate tiba sahihi
kwa kujengwa vizuri ili hata akirudi uraiani,
atakuwa na uwezo mzuri wa kujisimamia
mwenyewe kutokana na elimu atakayokuwa
ameipata,” alisema Msilo.
Kuhusu maendeleo ya Ray C ambaye hadi
Jumanne iliyopita alikuwa ametimiza takriban
siku tano kituoni hapo, meneja huyo ambaye pia
aliwahi kuwa muathirika wa madawa ya kulevya
kabla ya kutibiwa, alisema mrembo huyo kwa
sasa anaendelea vizuri.
Yeah! Ameanza vizuri tiba, anaendelea vizuri kwa
kweli. Naamini kadiri anavyoendelea atakuwa
vizuri zaidi. Kuna mabadiliko makubwa ameanza
kuyaonesha,” alisema Msilo huku akidai muda wa
kuwepo kwenye nyumba hiyo utategemeana na
jinsi Ray C atakavyoonesha kupona.
Akijizungumzia yeye kama mfano wa watumiaji
waliotopea na kisha kutibiwa, Msilo alisema licha
ya kuwa yeye alikuwa mwanajeshi kwa muda
mrefu, alijikuta ametopea kwenye madawa hayo
lakini tiba pekee iliyomfanya ajinasue kwenye
madawa hayo ni Sober House.
“Mimi nilikuwa mwanajeshi kwa takriban kama
miaka 10 na kitu lakini nilifukuzwa jeshi kutokana
na matumizi ya madawa ya kulevya, nikaenda
kutibiwa Kigamboni, kwa sasa nipo freshi kabisa.
“Naomba Mwenyezi Mungu anisimamie nisiweze
kurudia maana yeye ndiye anayetusaidia kuweza
kufikia malengo yetu, sisi tunapanga lakini yeye
ndiye anayetuwezesha,” alisema Msilo.
Kabla ya kufikishwa kituoni hapo, Ray C alipoanza
kuripotiwa na magazeti ya Global Publishers kwa
mara ya kwanza kuhusu kutopea kwenye
madawa ya kulevya, wadau mbalimbali waliguswa
na hali mbaya aliyokuwa nayo kitendo ambacho
kilimgusa rais mstaafu, Jakaya Kikwete
aliyemuita ikulu na kumsaidia.
Chanzo:GPL

Chapisha Maoni

 
Top