0
Baadhi ya mashabiki waliodai kuwa wanachama wa
klabu ya Simba, wamejitokeza kwenye mkutano wa
waandishi wa habari katika makao makuu ya klabu
ya Yanga na kuwataka Wanasimba kujitokeza kwa
wingi na kuiunga mkono Yanga, kesho.
Yanga inashuka dimbani kuivaa TP Mazembe
katika mechi ya Kombe la Shirikisho hatua ya
Makundi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam.
Amaniel Mngonja na Rifat Maulanga wamejitokeza
kwenye mkutano huo ulioongozwa na Msemaji wa
Yanga, Jerry Muro katika makao makuu ya Yanga,
Kaunda na Twiga jijini Dar es Salaam.
“Sisi sote ni mashabiki na wanachama wa Simba,
tunawaomba mashabiki na wanachama wenzetu
wajitokeze kwa wingi kuiunga mkono Yanga.
“Yanga ndiyo inayoiwakilisha Tanzania katika
michuano hiyo, hivyo waje kwa wingi kuishangilia,”
alisema Maulanga.
Kwa upande wake, Muro alisema kwa shabiki
ambaye hataweza kuvaa jezi za Yanga, angalau
avae jezi za Taifa Stars.
“Kama utashindwa basi vaa jezi ya Taifa Stars,
lakini bado unaweza kuvaa jezi ya timu yako hata
kama ni Simba lakini beba bendera ya taifa,
tuishangilie Yanga ni kwa ajili ya Tanzania.”
Kuhusiana na uanachama wa Simba wa Maulanga
na Mngonja, wote walikataa kutaja kadi zao za
uanachama na kusisitiza hawakuwanazo hapo.
Aidha Murro alitumia mkutano huo kusisitiza kuwa
klabu ya Yanga iliiandikia barua klabu ya Simba
juu ya kutaka ruksa ya kumtumia Hasan Kessy
kwenye michuano ya CAF.
Hapo jana Simba kupitia kwa Katibu Mwenezi
wake Haji Manara ilitoa taarifa kwa waandishi wa
Habari wakidai kuwa uongozi wa Yanga haujawahi
kuwasiliana nao kuhusu mchezaji huyo.
Simba ilidai kuwa haiwezi 'kuibania' Yanga
kumtumia mchezaji huyo kwa kuwa mwaka 1998
iliwahi kuiazima Yanga wachezaji watatu ili
waisaidie kwenye michuano ya klabu bingwa hatua
ya makundi.
Yanga imekwama kumtumia Kessy baada ya
Simba kugoma kuandika barua CAF kumuidhinisha
mchezaji huyo akipige katika michuano hiyo.
Simba inadai mkataba wa Kessy unaisha rasmi
Juni 30 hivyo Yanga italazimika kusubiri hadi
baada ya tarehe hiyo ndio waanze kumtumia
Kessy.

Chapisha Maoni

 
Top