Kocha Mkuu wa mabingwa wa Soka wa Ligi Kuu ya
Tanzania Bara Yanga, Hans van der Pluijm,
amesema iwe isiwe, kikosi chake hakitapoteza
mechi dhidi ya TP Mazembe kutoka Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inayotarajiwa
kufanyika Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa jijini
Dar es Salaam.
Katika mahojiano na gazeti la Nipashe, Pluijm
alisema kuwa anafahamu wazi kwamba akipoteza
pointi katika mchezo huo, atakuwa amejiondoa
kwenye mbio za kuwania ubingwa huo wa
mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu
huu.
Pluijm alisema kwamba licha ya mechi hiyo
kutarajia kuwa na upinzani, amewaondoa hofu
wachezaji wake kwa kutowaona TP Mazembe ni
bora zaidi yao.
"Ni mechi itakayokuwa na upinzani, lakini kwetu ni
muhimu kwa sababu tunahitaji kushinda, ushindi
utasaidia kuiweka timu katika nafasi nzuri kwenye
kundi, hakuna timu kubwa zaidi ya mwingine, timu
zote zilizoingia katika hatua ya makundi ni bora,"
Pluijm alisema.
Mdachi huyo alisema kuwa wachezaji wake
wanaendelea vizuri na mazoezi na amevutiwa na
kiwango kilichoonyeshwa na straika mpya wa timu
hiyo, Mzambia Obrey Chirwa ambaye amesajiliwa
kutoka klabu ya Platinumz ya Zimbabwe.
Naye mshambuliaji wa TP Mazembe Mtanzania
Thomas Ulimwengu amesema kikosi chao
kinatarajia kutua nchini kesho Jumapili tayari kwa
mchezo huo wa pili wa Kundi A.
Ulimwengu alisema wanakuja Tanzania kupambana
na kuhakikisha wanafanya vizuri, wameifuatilia
Yanga katika mechi zao mbalimbali za kuanzia
hatua ya awali ya mashindano ya Klabu Bingwa
Afrika na Ligi Kuu ya Bara.
"Hakuna mchezaji wa Yanga tunayemhofia,
tunakuja kucheza 'kitimu' kwa sababu tunakuja
kupambana na timu ya Yanga," Ulimwengu
alisema.
TP Mazembe ambao waliweka rekodi ya kuwa
klabu ya kwanza Afrika kucheza fainali za Klabu
Bingwa Dunia mwaka 2010 ndio inaongoza Kundi
A ikifuatiwa na Mo Bejaia ya Algeria, Yanga na
Medeama kutoka Ghana.
Mchezo huo utachezeshwa na refa Janny Sikazwe
kutoka Zambia ambaye atasaidiwa na Jarson
Emiliano dos Santos wa Angola na Berhe
O’Michael wa Eritrea huku Wellington Kaoma wa
Zambia atakuwa mwamuzi wa akiba. Kamishna wa
mchezo huo atakuwa Celestin Ntangungira wa
Rwanda.
Chapisha Maoni