0
RAIS Dk. John Magufuli amemtumbua
mfanyabiashara mmoja maarufu Dar es Salaam,
aliyebainika kufanya miamala ya fedha ya Sh
milioni saba hadi nane kwa kila baada ya dakika
moja.
Kutokana na hesabu ya Sh milioni saba
anayoingiza kwa dakika moja, mfanyabiashara
huyo hutengeneza Sh milioni 420 kwa kila saa
moja, sawa na Sh bilioni 5.2 kwa saa 12 na Sh
trilioni 16 kwa mwezi ambazo halipi Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT).
Rais Magufuli amesema mfanyabiashara huyo
aliyebainika kuwa na makampuni mengi, alikuwa
akishirikiana na Wakala wa Usajili wa Biashara na
Leseni nchini (BRELA) pamoja na Mamlaka ya ato
Tanzania (TRA).
Mkuu huyo wa nchi alitoa kauli hiyo Ikulu, Dar es
Salaam jana, baada ya kuwaapisha wakuu wapya
wa mikoa watatu katika hafla iliyohudhuriwa pia
na wakuu wa wilaya wateule.
Alisema waligundua jipu hilo baada ya kufuatilia
kwenye mapato.
“Tulikuwa tunafuatilia kwenye ‘revenue’ (mapato),
kwenye zile VAT ambazo zinatumika ‘ku-collect
revenue’ (kukusanya mapato), yupo mtu mmoja
ambaye alikuwa ametengeneza kampuni zake
nyingi, alikuwa anafanya ‘transaction’ (miamala)
ya fedha kila dakika moja kati ya Sh milioni saba
na nane.
“Na hizo risiti alikuwa anaziuza kwa
wafanyabiashara wengine, kwenye VAT anatakiwa
kulipia kwa asilimia 18. Wafanyabiashara wengine
hao walikuwa wanauziwa kwa asilimia tano na
wakishauza bidhaa wanakwenda kuomba TRA
iwarudishie hiyo asilimia 18, kwa hiyo Serikali
imekuwa ikipoteza asilimia 18.5, ni matrilioni na
matrilioni ‘of money’ (ya fedha).
“Bahati nzuri huyo mtu yuko kwenye mikono
salama, tunafuatilia namna tutakavyorudisha hizo
fedha, na huyo mtu alikuwa ana-connection kati
ya watu wa BRELA na TRA… hiyo ndiyo Tanzania.
“Najaribu tu kutoa mfano ili katika maeneo yenu
mkasimamie mapato ya Serikali, kwa sababu
tumepoteza mapato mengi kuliko tunavyofikiria,
huku Watanzania wakiteseka sana, na mambo
yanayofanyika ni ya ajabu,” alisema Rais Magufuli
akiwaambia wakuu hao wa mikoa na wilaya.
Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli
alisema mchakato wa kupata wakuu wapya wa
wilaya ulikuwa mgumu, na kwamba amewaacha
wengi wa zamani kwa kuwa hawakutimiza vigezo
alivyovitaka.
“Mchakato wa kupata ma-DC ulikuwa mgumu
kwa sababu ilibidi tuangalie historia ya kila
mmoja. Tuliangalia mambo mengi sana, lakini pia
tuliangalia kwa ku-preview atatimiza haya
tunayotaka kuyafanya kwa miaka mitano?
“Na ndiyo maana mnavyoona ma-DC wa zamani
waliorudi ni 39, kwa hiyo wale 101 wote
hawakurudi… niseme tu ukweli kwamba
hawakufikia vigezo tulivyokuwa tunavitaka,”
alisema Rais Magufuli.
Alisema katika uteuzi huo, alichukua wakurugenzi
kwa kuwa walifanya vizuri katika maeneo yao
waliyokuwa wakiyaongoza.
“Tulichukua wakurugenzi walio-perform vizuri
katika maeneo yao. Wapya wako takribani 100 na
waliobaki ni hao kati ya 38 na 39. Ni matumaini
yangu kwamba mtakwenda kufanya kazi na
kutimiza wajibu wenu.
“DC ni nafasi kubwa ya uongozi katika Serikali na
ndiyo maana mfano mkubwa wa DC mstaafu ni
Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), ni kwa sababu
alitimiza wajibu wake na leo yuko hapa,” alisema.
Mkuu huyo wa nchi aliwapa mikakati ya kufanya
kazi wakuu hao wa wilaya kwa kutimiza dhana ya
kuchapa kazi kwa niaba ya Serikali.
“Nina matumaini makubwa mtakwenda kutimiza
dhana ya kuchapa kazi kwa niaba ya Serikali,
ninyi ndio wawakilishi wetu na ndio mnawakilisha
wananchi wa maisha yote.
“Watanzania wana matatizo na changamoto
kubwa. Ni matumaini yangu kwamba
hamtaniangusha na hamtaiangusha Serikali. Nina
imani mtakwenda kutatua matatizo ya wananchi,
hasa walio masikini, sitegemei wala sifikirii
kwamba mkawe chanzo cha kutengeneza
matatizo,” alisema Rais Magufuli.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wasimamie haki,
huku wakimtanguliza Mungu katika kufanya kazi,
kusimamia maadili, kutenda haki, kutojihusisha
na rushwa, kuwatumikia Watanzania bila kubagua
dini, kabila wala vyama vyao.
“Kikubwa mkasimamie yale tuliyoyaahidi sisi
wanaCCM, kwa sababu wakati tunazunguka
tukiomba kura, yapo tuliyoyaahidi, hayo
mkayatekeleze kwa nguvu zote.
“Na wala asitokee mtu yeyote wa kuwakwamisha
kutekeleza hayo, ninyi ndio wakuu wa wilaya na
ninyi watatu ndio wakuu wa mikoa. Mna mamlaka
makubwa ya kuweka mahabusu mtu masaa 48
halafu kesho yake ukamwachia. Ila msiende
kuonea watu, mkachape kazi.
“Imani tuliyoionyesha kwenu sisi viongozi wenu
mkaionyeshe kwa Watanzania mnaowaongoza,
mkashirikiane na viongozi mtakaowaongoza,
wanasema umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.
“Nina uhakika mkisimama vizuri kwa kuzingatia
maadili mliyonayo, na bahati nzuri wengi mna
uzoefu katika maeneo yenu. Mkawahamasishe
Watanzania katika wilaya na mikoa yenu kufanya
kazi. Watanzania wengi tumezoea kulalamika,
tunataka tupewe, lakini hatufanyi kazi.
Tukawasimamie kuchapa kazi,” alisema.
Aliwataka wakuu hao wa wilaya ambao pia ni
wenyeviti wa kamati ya ulinzi na usalama,
kukemea rushwa katika maeneo yao na
kusimamia mapato ya Serikali.
“Huwa inatokea saa nyingine wakurugenzi kwa
sababu kuna fedha nyingi tunapelekaga kule,
wanadhani ni zao wakati ni za Serikali,
mkawasimamie bila woga.
“Kupitia halmashauri zenu, mkahakikishe fedha
hizo zinatumika kulingana na matakwa ya kanuni
na sheria za nchi,” alisema Rais Magufuli.

Chapisha Maoni

 
Top