0
Mhe. Kassim Majaliwa



Na Daudi Manongi
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa ameagiza
wakuu wa wilaya na mikoa kufanya ziara katika
maeneo yao hasa vijijini ili kujua matatizo ya
wananchi wao kwa ukaribu na kuyapatia
ufumbuzi.
Mhe.Majaliwa ameyasema hayo leo hii Ikulu jijini
Dar es Salaam wakati wakuu wa wilaya na mikoa
walipokuwa Ikulu wakila kiapo cha maadili ya
viongozi kabla ya kwenda kuapishwa na wakuu
wa mikoa yao.
Aidha Waziri Mkuu amesema kuwa wakuu wa
mikoa na wilaya waache kukaa maofisini mwao
badala yake watembelee wananchi na hasa wale
wa hali ya chini ili kujua matatizo yao ya Ardhi na
kupatia ufumbuzi migogoro ya wafugaji na
wakulima.
Pia Mhe.Majaliwa amewasisitiza wakuu hao
kutambua kwamba majukumu waliyonayo ni
makubwa na wananchi wana mategemeo
makubwa juu yao na hivyo ni budi wakatekeleza
wajibu wao na kuhakikisha watanzania wanapata
huduma zote za muhimu kwa kutumia elimu,
uwezo, uadilifu, uaminifu na uwajibikaji walionao
ili kufanikisha maendeleo kwa wananchi.
Aliongeza kuwa wakuu hao wana jukumu kubwa
la kusimamia pesa za serikali pesa za miradi
zinakokwenda katika halmashauri za wilaya zao
na kukazia kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua
kwa yeyote ambaye hatofanya kazi zake
kikamilifu.
Waziri mkuu amewaagiza wakuu wa Mikoa
kushirikiana kwa karibu na wakuu wa Wilaya ili
kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya maeneo yao
kwani wananchi wana kiu ya maendeleo katika
maeneo yao.

Chapisha Maoni

 
Top