0

Kampuni ya Azam Media imelitaka Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) kumalizana na klabu ya
Yanga kuhusu malipo ya fedha za zawadi za
ubingwa wa Kombe la Shirikisho (FA) msimu huu.
Tamko hilo la Azam Media inayomiliki kituo cha
runinga cha Azam Tv, limetolewa baada ya Yanga
kulalamika kutolipwa fedha hizo za ubingwa kiasi
cha Sh50 milioni.
Awali, kaimu katibu mkuu wa Yanga, Baraka
Deusdedit alisema anashangazwa na kitendo cha
TFF kutowalipa fedha hizo hadi sasa, tangu timu
hiyo ilipotwaa ubingwa mwezi uliopita kwa
kuifunga Azam FC mabao 3-1.
“Ni kweli hadi sasa hatujapewa fedha zetu za
zawadi ya ubingwa kiasi cha Sh50 milioni za
Kombe la FA. Tumefanya jitihada za kuzifuatilia
lakini hatupewi majibu ya kueleweka,” alisema
Baraka.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Media,
Rhys Torrington aliliambia gazeti hili jana kuwa,
kampuni hiyo ilishakabidhi fedha zote za udhamini
wa mashindano hayo kwa TFF, ambao ndiyo
waandaaji na wasimamizi, hivyo wao wanatakiwa
kutolea majibu ya hilo.
“Ni wajibu wa TFF kugawa fedha hizo za zawadi za
mashindano ya Kombe la FA. Sisi kama wadhamini
tumewekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye hayo
mashindano ikijumuisha na zawadi za washindi.
“Udhamini wetu sisi kama Azam kwenye hayo
mashindano ni kama ambavyo Vodacom
wanavyodhamini Ligi Kuu. Tukiwa kama
wadhamini wakuu wa mashindano, tunaweza
kuguswa kama kunakuwa na ugomvi kati ya Yanga
na TFF, lakini ni jukumu la pande hizo mbili
kutatua wenyewe matatizo yao,” alisema
Torrington.
Madai hayo ya Yanga yametolewa katika kipindi
ambacho timu zilizoshiriki Ligi Daraja la Kwanza
(FDL) bado zinaendelea kulilia kumaliziwa fedha
zao kiasi kisichopungua Sh3 milioni, zikiwa ni
udhamini wa makampuni ya Sahara Media na
StarTimes kwenye ligi hiyo.
Pia, zipo baadhi ya klabu zilizoshiriki mashindano
ya Kombe la Shirikisho ambazo mpaka leo
hazijalipwa fedha zao za ushiriki katika
mashindano hayo.
Akihojiwa na Kituo cha Redio cha Efm asubuhi
jana, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema
kama Yanga au timu nyingine yoyote ina madai
yake, yanatakiwa yawasilishwe kwenye ofisi za TFF
na siyo vinginevyo.
“Waje kwenye makao makuu ya TFF na
kuwasilisha madai yao. Hawapaswi kulalamika
huko kwenye vyombo vya habari. Walete hapa
malalamiko yao ili yashugulikiwe,” alisema Lucas.
Mwananchi


Chapisha Maoni

 
Top