Azam FC imefanikiwa kunasa saini ya winga nyota
wa timu ya Medeama ya Ghana, Enock Atta Agyei,
ambaye tayari amesaini mkataba wa miaka miwili
kujiunga na timu hiyo.
Kinda huyo anatua baada ya kulivutia Benchi la
Ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu, Zeben
Hernandez, ambaye amependekeza asajiliwe baada
ya kumuona kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam wakati Medeama ikiilazimisha sare ya bao
1-1 na Yanga katika mchezo wa Kundi A wa
Kombe la Shirikisho Afrika.
Uongozi wa mabingwa hao umefanya jitihada za
hali ya juu hadi kunasa saini yake, ambapo
umelazimika kumpandia ndege mshambuliaji huyo
hadi mjini Takoradi, Ghana, usajili huo ukiratibiwa
na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad
Kawemba, aliyeenda huko na kukamilisha vema
kazi hiyo maalumu kwa kuzungumza na pande
zote mbili mchezaji na uongozi wa Medeama
akiwemo Mmiliki wa timu, Moses Armah.
Akiwa nchini Ghana, Kawemba alipata fursa ya
kukutana na Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya
Ghana ‘Black Stars’, Avram Grant raia wa Israel,
wakati wa mchezo wa marudiano kati ya Medeama
na Yanga ulioisha kwa wenyeji kushinda mabao
3-1.
Katika mazungumzo yake na Kawemba, Grant
aliyewahi kuifundisha Chelsea na kuifikisha kwenye
fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2008,
aliipongeza Azam FC kwa kutambua kipaji cha
Enock na kumsajili.
“Nawapongeza sana Azam FC kwa kutambua kipaji
cha Enock akiwa amefikisha umri wa miaka 18,
nawaahidi nitakuwa namfuatilia kwa karibu kwa
kipindi chote cha mkataba wake atakachokuwa
Azam FC,” alisema Grant katika moja ya
mazungumzo yake na Kawemba.
Enock, 18, mwenye kipaji cha hali ya juu, mara
baada ya kukamilisha taratibu zote za kujiunga na
Azam FC, anatarajia kutua nchini kesho Jumamosi
saa 2.15 asubuhi na ndege ya Shirika la Ndege la
Kenya (KQ).
Winga huyo mwenye kipaji cha hali ya juu
anayetabiriwa kutikisa zaidi miaka michache ijayo,
ameanza kung’ara wakati akiwa hana uzoefu
mkubwa sana na Ligi Kuu ya Ghana kwani
amejiunga na Medeama Desemba mwaka jana
baada ya kufanya vizuri akiwa na Windy
Professionals ya Ligi Daraja la Kwanza nchini
humo.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB na
kinywaji safi cha Azam Cola, hivi sasa ipo kwenye
kambi Visiwani Zanzibar ikifanya maandalizi
kabambe ya kujiandaa na msimu ujao, kikosi
kikiwa chini ya makocha wapya kutoka nchini
Hispania.
Posted Africa News Sports
Chapisha Maoni