0

Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva, amesema
klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi, imedhamiria
kufuta aibu ya muda mrefu ya kutotwaa ubingwa
wala kushiriki michuano ya kimataifa na njia pekee
ni kufanya usajili makini.
Simba haijatia mguu miaka minne kwenye
mashindano ya soka ya kimataifa chini ya
mwamvuli wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari,
bosi huyo mkuu wa Simba alisema uongozi
umesikitishwa na hali ya kukosa mafanikio Simba.
Alisema miongoni mwa mambo yaliyowafanya
mashabiki wa klabu hiyo kutembea vichwa chini
kwa kipindi chote hicho usajili mbovu usiozingatia
mahitaji ya klabu kubwa kama Simba.
"Mafanikio ya timu ndani ya nje ya uwanja, siku
zote hutokana na maandalizi mazuri ikiwa ni
pamoja na kumiliki kikosi kizuri kinachoweza
kuleta ushindani kwenye michuano," alisema
Aveva na kuongeza:
"Kwa kipindi chote cha kufanya vibaya, Simba
hakuwa na wachezaji wa kiwango cha kuu. Safari
hii tunataka kufanya mambo kuwa tofauti na miaka
ya nyuma."
Alisema klabu imelazimika kuwa makini kufanya
usajili msimu huu, lengo likiwa ni kujenga kikosi
chenye wachezaji wa viwango vya daraja la
kwanza.
"Mashabiki na wanachama wasishangae kuona
tunaleta wachezaji wengi kutoka nje na kuwafanyia
majaribio, tunasaka wachezaji wenye uwezo wa
kuisaidia timu," alisema Aveva.
Alisema uongozi ungependa kuona timu hiyo
ikifanya vizuri Ligi Kuu msimu msimu huu na
kutwaa taji.
Katika hatua nyingine, Aveva alisema msimu wa
maadhimisho ya wiki ya klabu hiyo kuelekea siku
maalum ya klabu hiyo 'Simba Day' unaanza Julai
31.
Kilele cha maadhimisho yake itafanyika Julai 8 kwa
Simba kucheza dhidi ya Inter Clube inayoshiriki
Ligi Kuu ya Angola.
Timu hiyo inashika nafasi ya tano kwenye
msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 26 ikiwa
imecheza michezo 18.



Posted Africa News Sports

Chapisha Maoni

 
Top