0
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimelitaka Jeshi la
Polisi kuwapandisha mahakamani viongozi wake
wanaowashikilia kwa tuhuma za uchochezi
kisiwani Pemba.
Akizungumza na waandishi wa habari visiwani
hapa jana, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano
ya Umma wa chama hicho, Salim Bimani, alisema
kama polisi wana ushahidi wa viongozi wa CUF
na wafuasi wao kujihusisha na matukio ya
uvunjifu wa amani basi wawapeleke mahakamani.
Bimani alisema wanasikitishwa na hatua ya jeshi
hilo kuwaweka ndani viongozi na wafuasi wao
kwa muda mrefu bila ya kuwafikisha mahakamani
kinyume na haki za binaadamu.
“Tunalitaka Jeshi la Polisi kama wana ushahidi
juu ya viongozi wetu ambao wanawahusisha na
matukio ya uvunjifu wa amani kisiwani Pemba
basi wawapeleke mahakamani,” alisema Bimani.
Bimani alisema kuwa tokea kuanzishwa mfumo
wa vyama vingi Tanzania kumekuwa na
unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya raia hasa
wanachama wa CUF jambo ambalo alisema kuwa
linafanyika kwa nia ya kukikandamiza chama
hicho.
“Ikiwa sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo kila
wakati Zanzibar imekuwa ikishuhudia kuletwa
askari wengi katika kipindi cha uchaguzi,” alisema
Bimani.
Hata hivyo, alisema kuwa baada ya kumalizika
kwa uchaguzi wa Oktoba 25, 2015, kumekuwa na
hatua kadhaa za unyanyasaji dhidi ya wafuasi wa
chama hicho unaofanywa na vyombo vya ulinzi
na usalama.
“Haya yote yanayofanyika ili kuzima sauti za
watu, lakini tunawaambia viongozi wa CCM
pamoja na vyombo vya dola, tutaendeleza
msimamo wetu wa haki sawa kwa wote,” alisema
Bimani.
Alisema CUF inalaani vitendo vya hujuma dhidi ya
raia na mali zao unaofanywa kwa lengo la kuvipa
sababu vyombo vya ulinzi na hasa wafuasi wake,
pamoja na kulaani kauli za vitisho na lugha za
kibabe zinazotolewa na Jeshi la Polisi Zanzibar,
kama vile iliyotolewa Juni 28 mwaka huu na
Naibu Mkurugenzi wa Upepelezi Salum Msangi
kisiwani Pemba kwa lengo la kuwanyamazisha
wananchi ili kuisambaratisha CUF.

Chapisha Maoni

 
Top